MZEE SOMBI : VIJANA WANAOGOPA KUOA KWA SABABU HAWANA KAZI....HAWATAKI USUMBUFU

Mzee James Makungu Sombi akizungumza na Malunde1 blog leo Jumatatu Oktoba 28,2019 


Na Kadama Malunde - Kisesa

Wimbi la vijana kutooa ama kuolewa limekuwa likiongezeka kila kukicha kutokana na vijana kutofanya kazi za kuwaingizia kipato hivyo kuona jambo la kuwa na familia ni mzigo na usumbufu katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na Mzee maarufu wa Kabila la Kisukuma James Makungu Sombi (85) mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza wakati akizungumza na Malunde1 blog ambapo amesema kutokana na vijana kuwa wazembe,kutaka kula tu na kuzurura ndiyo maana suala la kuoa au kuolewa linakuwa gumu. 

“Msichana hana kazi,mvulana hana kazi unadhani wakianza kuishi pamoja nyumba itakalika?.Kijana hana kazi atamlisha nini mke wake?,pesa za kumvalisha zitatoka wapi?,ndiyo maana vijana hawaoi ili kukwepa majukumu ya familia kwani akioa atakosa raha akiwaza atapata wapi pesa za kutunza familia”,amesema Mzee Sombi. 

“Zamani kilimo ndiyo ilikuwa ngao nzuri ya kumuweka mtu katika maisha mazuri,lakini siku hizi vijana hawataki kulima,hata kufanya kazi nzito nzito hawataki,ukimwambia kijana akalime unakuwa kama umemfukuza, wanakimbilia mjini,wao wanataka kula na kuzurura tu,sasa mtu wa namna hiyo ataoa kweli?”,alihoji Mzee Sombi. 

“Zamani huku kwetu tulikuwa na Shikome,hii ilikuwa kama ofisi ya mambo mbalimbali,wazazi walitumia shikome kuongea na vijana wao,lakini siku hizi hakuna shikome,wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto wao na watoto nao hawataki kushauriwa na wazazi, matokeo yake tunakuwa na vijana wa hovyo kweli kweli”,amesema. 

Anasema tofauti na sasa zamani wazazi walikuwa wanawatafutia vijana wachumba wa kuoa kisha kijana anaenda kuhakikisha kama mchumba anafaa ndipo anaoa lakini siku hizi vijana wanajiamulia wao wenyewe ndiyo maana hata ndoa hazidumu. 

“Kijana kajiamulia mwenyewe kuoa,msichana kakubali kuolewa,msichana yupo ndani ya ndoa akiona kijana huyo hana kazi anafikiri ataishije,mwisho wa siku kwa kuwa naye hana kazi anaamua kuondoka kwenda kutafuta pesa mahali pengine, na kama walibahatika kuzaa basi mtoto anajikuta analelewa na mzazi mmoja na mara nyingi mtoto atakuwa hana maadili na huo ndiyo mwendelezo wa kuwa na vijana wasio na maadili”,ameelza 

Mzee Sombi anasema zamani wanandoa walikuwa wanavumiliana kwa sababu hawakuwa na tamaa ya kupata pesa wao nia yao ilikuwa ni kupata familia na kuzaa na kulea watoto wao. 

“Wasichana wetu siku hizi wakiona wamepata mtoto wanawaza kwamba huyu mtoto atamlisha nini ndiyo maana wengine wanaamua kuwatupa ili wapate nafasi ya kwenda kutafuta pesa kwa wanaume wengine,nawashauri wanawake wawe wanajishughulisha ili wapate kipato badala ya kutegemea wanaume ambao mara nyingi wamekuwa wakiwakimbia na kujikuta tunakuwa na Single Mother wengi 'familia ya mama na mtoto'”,alisema Mzee Sombi.

Mzee James Makungu Sombi ambaye ni mkazi wa Kisesa Mwanza ni Manju Mstaafu wa ngoma za Kisukuma na ni miongoni mwa waanzilishi wa Makumbusho ya Kisukuma ya Bujora yaliyopo Kisesa jijini Mwanza

Mzee Sombi ni Mtaalamu wa Masuala ya Utamaduni wa Kabila la Kisukuma,Wasiliana naye kwa namba 0755903972

KUFANYA SANA MAPENZI KUNAPUNGUZA SIKU ZA KUISHI....BABU WA MIAKA 85 ATOA USHAURI

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527
Previous Post Next Post