JAFO ATOLEA UFAFANUZI MALALAMIKO YALIYOWASILISHWA KWENYE ZOEZI LA UCHUKUAJI NA UREJESHAJI WA FOMU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo ametolea maelekezo malalamiko yaliyowasilishwa na wadau wa uchaguzi kuwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi za uongozi uzingatie Kanuni za uchaguzi na miongozo iliyotolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni Ofisini kwake Mtumba Jafo ameelekeza Wasimamizi/Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi, Vyama vya Siasa na wadau wengine woote kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anazingatia masharti na miongozo iliyotolewa kuhusiana na uchukuaji na urejeshaji wa fomu.

Amebainisha baadhi ya malalamiko yaliyowasilishwa toka kwa vyama vya siasa kuwa ni kutokuwepo vituoni kwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi, baadhi ya wasimamizi kutofungua kwa wakati vituo vya kuchukulia fomu, mihuri na masuala mengine ya Kikanuni.

“Malalamiko yaliyopokelewa yanaendelea kufanyiwa kazi, hata hivyo wadau na vyama vya siasa wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati za rufaa zilizopo katika maeneo ya uchaguzi,” alibainisha.


Akieleza maendeleo ya uchaguzi huo jana jijini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, alisema dosari zilizojitokeza ni chache kwenye baadhi ya mikoa.

Alisema katika Kata 3,959 ni kata 72 pekee ndizo amepokea malalamiko na kutaja maeneo machache kama vile Songwe, Lindi, Sengerema (Mwanza) na Moshi (Kilimanjaro).

Hata hivyo, Jafo alisema malalamiko kuhusu fomu zinazotolewa kwa wagombea kutogongwa muhuri, vyama vya siasa vinapaswa kufahamu kuwa, zitagongwa muhuri   pindi watakaporudisha au wakati wa uteuzi.

Kadhalika, alitoa msisitizo kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi kuzingatia kanuni za uchaguzi kama zilivyowekwa.

Juzi, Waziri Jafo alitangaza wagombea kwenye uchaguzi huo kuanza kuchukua fomu kwenye ofisi za wasimamizi wa uchaguzi hadi Novemba nne mwaka huu.

Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti wa Mtaa, Kitongoji, Kijiji, Wajumbe wa Kamati ya  Mtaa, Waju,mbe wa Serikali ya Kijiji.

Uchaguzi huo ambao ni wa sita tangu kuanza mfumo wa vyama vya siasa nchini, unatarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu ambapo wapigakura zaidi ya milioni 19 wanatarajiwa kushiriki



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527