HABINDER SINGH SETH KAANDIKA BARUA KWA DPP KUKIRI MAKOSA YAKE

Mfanyabiashara maarufu , Habinder Singh Seth ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.


Wakili wa Seth, Michaele Ngalo, ameiarifu Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Oktoba 10 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Seth pamoja na mfanyabiashara mwenzake James Rugemalira,  kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 wanayodaiwa kuyatenda jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hiyo Juni 19, 2017 na hadi sasa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi na kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya Dola milioni 22 na Shilingi za Tanzania bilioni 309.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amethibitisha kuwa wamepokea barua ya Seth wanaifanyia kazi na majibu yatatolewa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 24, 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527