BILIONI 10 ZA RAIS MAGUFULI ZAANZA KAZI RUVUMA

Na Mwandishi Wetu,Ruvuma
Shilingi Bilioni 10 zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka huu na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba za Askari wa Vyeo vya chini zimeanza kutumika mkoani Ruvuma huku jumla ya nyumba sita zikiwa zimejengwa katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.


Rais Magufuli aliahidi kutoa kiasi hicho cha fedha wakati akizindua Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia jijini Arusha mwezi April mwaka huu.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya ukaguzi wa nyumba hizo mkoani Ruvuma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni alisema tayari nyumba hizo zimekamilika na tayari ujenzi unaendelea mikoa yote nchini ambako ilibainika kuna changamoto ya makazi ya askari

“Rais wetu aligundua changamoto ya askari wetu hawa hasa wa vyeo vya chini,akatoa kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa jeshi la polisi,leo nimefika hapa kuangalia matumizi ya fedha hizo na nimeridhishwa na hatua ya ujenzi ulikofikia kwani nyumba zimekamilika na tayari nimeona baadhi askari wetu washahamia,”alisema Masauni

“….tunatembea nchi nzima kuona nyumba hizo zimefikia hatua gani lengo ni kuona askari wetu wanahama katika makazi duni na kuhamia nyumba hizi mpya ambazo serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa hiyo changamoto.” Aliongeza Masauni

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,Kamishna Msaidizi Simon Marwa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kiasi hicho cha fedha ambapo wao walipata mgao wa Shilingi Milioni 150/=  huku akitaja idadi ya nyumba walizojenga.

“Nyumba zishakamilika na askari wa vyeo vya chini wameshahamia kama maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalivyosema, hapa kuna nyumba sita ambazo kuna vyumba viwili vya kulala, sebule na chumba cha kulala kwa kila nyumba,” alisema RPC Simon

Kamanda Simon alisema mkoa wa Ruvuma una wilaya tano za Songea, Tunduru, Mbinga, Namtumbo na Nyasa huku mapendekezo ya nyumba hizo kwa mkoa huo zikijengwa wilayani Namtumbo ambako changamoto ya makazi ilikua kubwa tofauti na wilaya zilizobakia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527