BASHE: TUNAHITAJI TAFITI BORA ZA MBEGU

Na Bashiri Salum, Wizara ya Kilimo,Morogoro

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo  Hussein Bashe jana (10/10/2019 ) aemeshauri Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na Wakala wa Uzalishaji Mbegu Tanzania (ASA) kushirikiana kuzalisha mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya wakulima.

Amesema taasisi za Serikali zinapasa kuwa mdau wa kwanza katika kuhakikisha mbegu bora na za kutosha zinapatikana.

“Usalama wa Chakula utakuwa endelevu endapo hatua madhubuti zitachukuliwa kuona taifa linazalisha mbegu za kutosha na zinazohimili magonjwa” alisema Naibu Waziri

Bashe yupo mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi kukagua shughuli za uzalishaji mbegu ambapo alifanya mikutano na wakuu wa Viongozi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine,Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) pamoja na Wakala wa Mbegu (ASA)

Bashe alisitiza kuwa uchumi hauwezi kukua kama hakutakuwa na uwekezaji mzuri  kwenye kilimo kwa kutumia utaalam unaopatikana kwenye taasisi za kitaaluma.

Naibu Waziri alibainisha kuwa ni lazima kilimo kiangaliwe  kwa jicho la kibiashara ili kiweze kumvutia mkulima na wawekezaji hivyo ni wakati wa wataalamu wa kilimo  kuchochea mabadiliko chanya.

“Ni muda muafaka sasa tafiti nyingi za SUA zitokane  na matatizo ya wakulima ili waweze kuzitumia na kubadilisha kilimo chao kuwa chenye tija” alisema Bashe

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof Raphael Tihelwa Chibunda amesema chuo chake kipo tayari kufuata maelekezo kwa kuwa tafiti zao zote zinalenga mahitaji ya jamii ya watanzania.

Prof Chibunda amesema pamoja na kuongeza uzalishaji wa mbegu lakini ni muhimu kama nchi kuimarisha huduma za ugani ili kuleta matokeo mazuri pindi wakulima watakapotumia mbegu bora za kilimo

Hata hivyo amemweleza Naibu Waziri kwamba imefika wakati nchi kuondokana na kuweka vikwazo zadili (regulatory) badala yake iwe na mikakati ya  promosheni kwa kuwa bado hatujawa na utoshelevu katika mbegu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527