BASHE : SERIKALI ITALINDA SOKO LA NDANI LA PAMBA

Na Bashiri Salum, Wizara ya Kilimo

Serikali imesema inatakutana na wadau wa zao la pamba nchini mapema mwanzoni mwezi Novemba mwaka huu ili kujadili changamoto zilizopo za ukosefu wa soko la uhakika na upatikanaji wa viwanda vya kuchakata zao hilo.


Hayo yamesemwa jana (11.10.2019) na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati alipotembelea kiwanda cha Twenty One Century cha mjini Morogoro kukagua uzalishaji wa bidhaa za pamba.

Akiwa katika kiwanda hicho Naibu Waziri Bashe alibaini changamoto ya kiwanda kuzalisha bidhaa za pamba tani 24,000 kwa mwaka ambazo hazilingani na uzalishaji uliopo nchini.

“Kiwanda cha Twenty one Century ambacho ndicho chenye uzalishaji mkubwa kati ya viwanda vyote vya nguo hapa nchini lakini kinatumia tani elfu 24 tu za pamba kwa mwaka.” alisema Bashe .

Alibainisha kuwa wakulima mwaka huu wanategemea kuzalisha zaidi ya tani 700,000 tofauti na mwaka jana zilizalishwa takribani tani 400,000 hivyo kunahitajika viwanda vingi zaidi ili mkulima apate soko la uhakika.

Bashe amesema mkakati wa serikali ni kuona viwanda saba (ginnery) za Lugulu,Sola, KACU, Mbogwe, Chato, na Manawa zilizopo katika ukanda unaolima zao la pamba kwa wingi vinafufuliwa haraka.

Mkutano ujao wa wadau utawakutanisha Wawekezaji wa viwanda vya pamba ,Wachakataji wa pamba (Ginnery), Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara na Viongozi wa Vyama vya Ushirika ili kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya pamba nchini.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Bashe amepokea malalamiko ya wawekezaji wa viwanda vya pamba kuhusu uwepo wa kanga na vitenge vinavyoingizwa nchini vikiwa na ubora hafifu toka nje , hali inayochangia kushusha bei ya bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.

Naibu Waziri huyo ameahidi kufanyia kazi malalamiko haya ili kulinda soko la ndani na kuwezesha lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha uchumi wa viwanda linafanikiwa kwani malighafi ya viwanda inapatikana kwa wingi toka kwa wakulima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527