WAZIRI WA KILIMO JAPHET HASUNGA AFANYA MAZUNGUMZO NA MTENDAJI MKUU WA KAMPUNI YA INNOVATION AFRICA

Na Mathias Canal, Telaviv-Israel

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)  tarehe 4 Septemba 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovation Africa Bi Sivan Ya’ari.

Katika kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ofisi za kampuni hiyo zilizopo Jijini Tel Aviv nchini Israel, Mhe Hasunga amemualika Bi Sivan kutembelea nchini Tanzania ili kuwekeza kadhalika kusaidia katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Alisema kuwa kampuni hiyo inatakiwa kuongeza mshikamano na serikali ya Tanzania ili kuendelea kutatua sehemu ya matatizo ya wananchi huku kuimarisha mpango wao wa kutoa suluhisho la Israeli na ujuzi kwa wale wanaohitaji kuishi katika vijiji vya Kiafrika.

Waziri Hasunga amemuhakikishia Bi Ya’ari kuwa Tanzania ni nchi nzuri katika uwkeezaji na sehemu salama ya kuishi huku serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ikiendeleza juhudi za kuboresha maisha ya watanzania na kuimarisha uchumi wa nchi.

Hata hivyo ameipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi za Afrika katika sekta ya nishati ya jua ikiwa ni pamoja na mchango wao katika kutekeleza miradi ya maji safi, na Kusaidia vituo vya watoto yatima.

Alisema kuwa Tanzania ni sehemu salama na imara katika uwekezaji, kwani serikali imeanzisha kituo cha uwekezaji (TIC) ambacho ni Taasisi ya msingi ya serikali yenye jukumu la kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji.

Tanzania inaongoza kwa uwekezaji katika Afrika Mashariki na imeweza kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda dola za Marekani bilioni 0.7 na Kenya dola za Marekani bilioni 0.67. “Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki

Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imebainisha kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji huku Taarifa nyingine ya“The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.”

Kwa upande wake Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovation Africa Bi Sivan Ya’ari akizungumza katika kikao kazi hicho ameridhia ombi la Waziri Hasunga la kuongeza uwezekano wa kuisaidia Tanzania na kusema kuwa mwanzoni mwa mwezi wa tisa atawasili nchini Tanzania kwa ajili ya kuainisha maeneo ya uwekezaji.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga yupo katika ziara ya kikazi ya siku sita nchini Israel ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Agro Studies ambapo miongoni mwa mazungumzo muhimu itakuwa ni pamoja na kumuomba uwezekano wa kuongezewa nafasi zaidi ili vijana wengi wa kitanzania waende kujifunza mbinu mpya za kilimo nchini Israel.

Pia, Mhe Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo nchini Israel kujadiliana nae maeneo mbalimbali na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania

MWISHODownload/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post