WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA WITO WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema mabadiliko ya tabianchi ni janga la kitaifa na dunia kwa ujumla hivyo kila mtu anao wajibu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti.

 
Mhe. Simbachawene amesema hayo leo Septemba 6, 2019 wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Alisema kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi imesababisha mabadiliko ya misimu na hivyo kuleta athari kwa wanadamu kushindwa kuendesha shughuli za kilimo.

"Hali hii imechangia sana kubadilisha misimu mbalimbali kwani baadhi ya mazao tuliyozoea hatuyapati tena kutokana na kukosekana kwa mvua na pia mifugo yetu inakosa malisho yote haya yanasababisha kwa mabadiliko ya tabianchi," alitahadharisha.

Waziri Simbachawene alibainisha kuwa takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanategemea mvua kufanya shughuli za kilimo lakini Tanzania inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.

 Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya nchi ilikuwa na ukame ambao ulichangia uzalishaji mdogo wa mazao na Serikali lichukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwataka wananchi kutumia chakula kwa uangalifu, kupanda mazao yanayohimili ukame, kuuza mifugo ili kununua chakula na kuhifadhi

Waziri Simbachawene alibainisha kuwa kwa mujibu wa sheria suala la utunzaji wa mazingira si tu la Ofisi ya Makamu wa Rais bali ni la kila mmoja ambapo taasisi zingine za Serikali na zisizo za Serikali zinapaswa kushiriki ili kuhakikisha tunaondokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha Waziri Simbachawene alipongeza miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ya Eco villages ambayo imetekelezwa katika maeneo kadhaa nchini na kusema itapunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kuwa miradi hiyo iliyotekelezwa imeweza kuwajengea uwezo wananchi kuhusu namna ya kufanya shughuli mbadala pale panapokuwa na changamoto za kimazingira kama hizo na hivyo kujikimu kimaisha.  

Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo cha Mipango Dodoma kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali likil;enga kujadili taarifa za miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527