WAZIRI JAFO ATOA ONYO.....AWATAKA WAKURUGENZI WAWE MAKINI NA WASIMAMIE MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Na. Angela Msimbira OR -TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa weledi fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.



Ameyasema hayo jana wakati akifungua semina ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi  wa Halmashauri na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa  iliyofanyika katika Ukumbi  wa Auditoriumn, Chuo Kikuu cha Dodoma, Jijini Dodoma.

Mhe. Jafo amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua Wakurugenzi ambao wataenda kinyume na utaratibu wa matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa kukuika miongozo iliyotolewa na Serikali katika matumizi sahihi ya fedha hizo.

Mhe. Jafo ameonya matumizi yasiyofaa kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na kusisitiza kuwa fedha hizo ni za moto, hivyo matumizi yake yanahitaji kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Ameendelea kusema kuwa ni marufuku kwa Mkurugenzi kutumia fedha za uchaguzi kinyume na agenda ya uchaguzi na kusisitiza haja ya fedha hizo kutumika kwa wakati.

“Naomba niwape tahadhari, katika matumizi ya fedha ya uchaguzi, fedha hizi za uchaguzi zinazokuja ni kwa ajili ya uchaguzi, naomba mtu asidanganyike wala kurubunika kwa lolote katika mchakato huu wa uchaguzi, katika fedha za moto hizi fedha za moto” Amesisitiza Mhe. Jafo

Mhe. Jafo amesema kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inasimamia kwa karibu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivyo ni matumaini kuwa matumizi ya fedha za uchaguzi zitaenda kama ilivyokusudiwa kwa kufuata miongozo ya matumzi ya fedha hizo.

Amesema kuwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini  ndio wenye dhamana ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kinyume na hapo anapaswa kujibu hoja zitakazojitokeza za kushindwa kusimamia fedha hizo vizuri.

Kuhusu wasimamizi wa uchaguzi, Mhe. Jafo amewasihi kutekeleza makujukumu yao kwa weledi na kuhakikisha ratiba ya uchanguzi inafuatwa huku akiwataka kutambua kuwa wasimamizi wamebeba dhamana kubwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia Demokrasia.

“ Natamani sana mlioteuliwa kuwa wasimamizi wa uchaguzi mwende vizuri mpaka mmalize vizuri kwa mujibu wa kanuni zetu. Mheshimiwa Rais anatamani nchi yake ikatekeleze demokrasia vizuri na ndio maana mnaona ameweza kuwezesha kila eneo kwa lengo kuwa uchaguzi uende ukafanyike vizuri”. Amesema Mhe. Jafo

Amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini ni muhimu kwa kuwa maisha ya watu yanaanzia katika vitongoji, mitaa na vijiji vyenu, mustakabali wa kuchakata maendeleo lazima uanze katika ngazi husika ambayo uchaguzi huu unaenda kuwapata viongozi na  hawawezi  kupatikana kama wasimamizi wa uchaguzi mtashindwa kufanya kazi yenu vizuri.

Wakati Huohuo, Mhe Jafo amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa ambao ndio waratibu wakuu wa uchaguzi kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu kila tukio na kuwataka wasikubali kuharibiwa kazi.

 “Makatibu Tawala wa Mikoa wao ni waratibu wakuu wa Uchaguzi katika Halmashauri zao kipindi hiki mna kazi kubwa sana ya kuhakikkisha huko chini mambo yanaenda vizuri na wala msikubali hata kidogo mtu awaahiribie kazi”. Amesisitiza Mhe. Jafo

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameeleza kuwa kikao hicho kinalenga kukumbushana majukumu ya uchaguzi huo na kuna matukio mbalimbali yaliyopo katika tangazo la uchaguzi yanayopaswa kutekelezwa.

Mhandisi Nyamhanga amesema OR-TAMISEMI imeshakamilisha maandalizi yote muhimu ya uchaguzi huo na nyaraka mbalimbali zimeandaliwa na kusambazwa ikiwemo kanuni na muongozo wa uchaguzi huo.

Amesema tayari  imeratibu upatikanaji wa fedha na tayari zimeshatumwa kwenye Sekretarieti za Mikoa yote na anaamini zimeshatumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya maandalizi.

Aidha, Nyamhanga alisema katika uchaguzi wa mwaka huu inakadiriwa kuwa na vituo vya kupigia kura 110,000.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527