WAZIRI HASUNGA: TUTAFANYA MABADILIKO MAKUBWA KWENYE SEKTA YA KILIMO

Na Mathias Canal, Telaviv-Israel

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali YA Tanzania imejipanga kuikabili sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwaandaa watanzania katika kubadilisha kilimo chao kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara.

Waziri Hasunga ameyasema hayo  tarehe 3 Septemba 2019 wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Tel Aviv nchini Israel.

Alisema kuwa katika ziara yake hiyo amejifunza namna ambavyo nchi ya Israel imepiga hatua ya ujuzi katika sekta ya kilimo hivyo kuona umuhimu wa serikali ya Tanzania kuwekeza katika skimu za umwagiliaji.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya wakulima nchini Tanzania wanatumia majembe ya mkono katika kilimo jambo ambalo haliwezi kuongeza tija na uzalishaji. “Tunatumia majembe ya mkono mbaya zaidi kilimo chetu kinategemea msimu wa mvua, hivyo kilimo cha namna hiyo bado kinatuchelewesha, tuna wajibu wa kujifunza kwa wenzetu walioendelea” Alisema Mhe Hasunga

Alisema kwa kuanza serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa kilimo inaweza kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uwezo wa kilimo cha umwagiliaji kitakachofanya kazi msimu mzima badala ya kilimo cha kutegemea mvua.

Mhe Hasunga alisema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kadhalika wizara ya Viwanda na Biashara zitafanya kazi kwa pamoja ili kuona namna ya kuzalisha kwa tija mazao ya kilimo na kutoa malighafi nyingi zitakazochangia katika kuinua na kuchagiza matakwa ya serikali ya kuwa na serikali ya viwanda.

Kuhusu masoko ya mazao yanayozalishwa nchini Tanzania Mhe Hasunga alisema kuwa serikali inaendelea na mkakati maalumu wa kuimarisha masoko kwani imeanzisha kitengo maalumu katika wizara ya kilimo kitakachokuwa na wajibu wa kushughulikia masoko ya mazao ya wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameyaalika makampuni mbalimbali ya Israel yanayojishughulisha na kilimo kutembelea nchini Tanzania kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

“Tanzania ni nchi yenye rutuba nzuri, eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo, hivyo nayaalika makampuni yote yanayohusika na kilimo hususani yanayojishughulisha na utafiti, kutembelea Tanzania kwani ni nchi yenye eneo zuri na kubwa kwa ajili ya uwekezaji hususani katika sekta ya kiliumo” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe Hasunga amesema kuwa Israel ni nchi yenye eneo dogo kwa ajili ya kilimo lakini wanazalisha chakula kinachotosheleza wananchi wake sambamba na kuuza mazao yao nje ya nchi jambo ambalo linaimarisha pato la serikali ya nchi hiyo na kipato cha mtu mmoja mmoja.

Vilevile, waziri Hasunga ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Israel unaoongozwa na Mhe Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima na watendaji wengine wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uwakilishi wa Tanzania, Aidha Mhe Hasunga amemuomba Balozi huyo kutafuta fursa zaidi za makampuni ya kilimo na viwanda kwa ajili ya kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu ya kuyafanyia kazi ni pamoja na kutafuta namna ya kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki katika mafunzo ya kilimo ya Agro Studies ili izidi kuongezeka maradufu.

Kadhalika, alisema kuwa ofisi yake inaendelea kufanya kazi kubwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini Tanzania kwani idadi kubwa ya watalii inaongeza pato la kigeni la nchi.

Balozi Masima alisema kuwa nchi ya Israel ina mafanikio makubwa kwenye sekta ya teknolojia hivyo ni wajibu wa Tanzania kutumia fursa hiyo muhimu katika elimu ya ujuzi wa teknolojia za kilimo hususani umwagiliaji.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post