WALIOKUWA WAFANYAKAZI NA WATEJA WA BENKI YA FBME KULIPWA AMANA

Na. Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma

SERIKALI imeeleza kuwa itawalipa waliokuwa wateja na wafanyakazi wa Benki ya FBME baada ya taratibu za kisheria na majadiliano na Cyprus yatakapo kamilika hivi karibuni.

Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali ya Mhe. Jaku Ayoub, aliyetaka kujua Benki ya FBME ipo katika hali gani na ni lini italipa wateja amana zao.

Dkt. Kijaji alisema kuwa wateja wa Benki ya FBME waliokuwa na amana ya milioni 1.5 Serikali imewalipa kwa zaidi ya asilimia 83 ya wateja wote, asilimia 17 iliyobaki ni ya wateja ambao hawajajitokeza kuchukua amana hizo.

“Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board- DIB) ilianza zoezi la kulipa fidia kwa mujibu wa sheria kwa waliokuwa na amana katika benki hiyo kuanzia Novemba, 2017 na bado zoezi hilo linaendelea”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa hadi kufikia Septemba 9, 2019 jumla ya kiasi cha Sh. milioni 2,404.2 kimelipwa kwa wateja 3426 kama fidia ya bima ya amana, ambapo kiasi hicho ni sawa na asilimia 55.9 ya kiasi chote kilichotarajiwa kulipwa kama fidia ya bima ya amana kwa wateja wote 6,628 waliopo Tanzania na wateja waliopo nje ya nchi (Tanzania International Banking Depositors- TIB)

Aidha jumla ya Sh. milioni 2,401.2 zimelipwa, ikiwa ni asilimia 83.3 ya lengo la kulipa jumla ya Sh. milioni 2,882.6 kwa wateja waliopo Tanzania tu.

Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amempongeza Mwanasheria na Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuhakikisha amana za wateja FBME ambao wako ndani na nje ya nchi zinabaki salama na kuzipata baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 imeipa Benki Kuu ya Tanzania- BOT, mamlaka ya kutoa leseni, kutunga kanuni, kusimamia benki zote zinazochukua amana za wateja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya benki zinazoendesha biashara bila kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

 Kwa ujumla Benki Kuu imepewa mamlaka ya kusimamia na kudhibiti benki na taasisi za fedha ili kuhakikisha kuwa amana za wateja zinakuwa salama na pia kuna usalama, utulivu na uthabiti wa sekta ya fedha na uchumi.

Benki ya FBME Ltd ilifutiwa leseni ya kufanya biashara hapa Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania Mei 8, 2017 kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya kutakatisha fedha nchini Marekani.

Benki  Kuu nchini Tanzania iliiteua Bodi ya Bima ya Amana- DIB kuwa mfilisi wa Benki ya FBME, hivyo kwa sasa  benki hiyo haiendeshi shughuli zozote za kibenki hapa nchini.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post