WALIMU WAWILI JELA MIAKA 30 KWA KUMBAKA MWANAFUNZI KWA ZAMU


Walimu 2 wa Sekondari Wilayani Iramba, Singida wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kukutwa na hatia ya kumbaka kwa zamu Mwanafunzi wao wa kidato cha pili(15).

Waliohukumiwa ni Ernest Emmanuel (25) na Onesmo Bida (28), huku wenzao wawili ambao pia wanatuhumiwa kumbaka mwanafunzi huyo, kesi yao bado inaendelea.

Walimu hao wanne, wanadaiwa kumbaka mwanafunzi huyo kwa zamu huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria namba 130 kifungu (1) kifungu kidogo (2) (E) kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lyoba Mkambala, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Iramba, Makwaya Charles, kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti toka Machi 2 mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

Mkambala alidai mshtakiwa Ernest Emmanuel, alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na dada wa mwanafunzi huyo.

Alidai Machi 20 mwaka jana, saa 2 usiku, mwanafunzi huyo alienda nyumbani kwa shemeji yake Emmanuel kwa lengo la kuangalia sinema (movie).

“Baada ya kumaliza kuangalia ‘movie’, mwanafunzi huyo aliamua kurejea kwenye nyumba ambayo alikuwa amepanga. Mwalimu Emmanuel aliamua kumsindikiza na kuingia naye chumbani.

“Mwanafunzi alimbebeleza mwalimu wake ambaye pia ni shemeji yake arudi kwake ili yeye aweze kujisomea, lakini mwalimu alikataa na kisha kumshika kwa nguvu na kumwingilia kimwili,” alidai Mkambala.

Alidai kuwa Januari 21, mwaka huu, wazazi wa mwanafunzi huyo walimchukua binti yao na kwenda naye hadi kwa mkuu wa shule kushtaki kwamba mtoto wao anakataa shule.

“Mwanafunzi huyo baada ya kuhojiwa, alisema ana mimba. Pia alitumia nafasi hiyo kutaja walimu waliomwingilia kimwili kuwa ni Ernest Emmanuel, Onesmo Bida, Keneth Komba na Ally Pangu, aliosema kila mmoja alimbaka kwa muda wake,” alidai.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527