MWANDISHI WA HABARI SEBASTIAN ATILIO AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUANDIKA UONGO FACEBOOK

                                        Sebastian Atilio


Mwandishi wa habari wa kujitegemea anayeandika habari zake katika ukurasa wa kitabu sura (Face Book) katika wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa Sebastian Atilio amefikishwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Mufindi kwa makosa mawili likiwemo la kuandika habari za uongo na kufanya kazi bila kusajiliwa na bodi anaripoti mwandishi Francis Godwin kutoka mkoani Iringa.

Akisoma mashtaka haya leo Jumanne Septemba 10,2019 mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Edward Uforo ,mwendesha mashitaka wa Jamhuri Victor Kitamale alisema kuwa Sebastian anashitakiwa kwa kosa la kwanza kufanya kazi bila kusajiliwa katika bodi ya uandishi na kosa la pili ni kuandika habari za uongo juu ya wananchi wa kijiji cha Ifupila kuhamishwa.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alikana mashitaka yote yanayomkabili huku mahakama hiyo ikisema kuwa makosa hayo kisheria yana dhamana.

Wakati mwendesha mashtaka wa Jamhuri alipinga dhamana hiyo chini ya kifungu namba 148(5) D) cha sheria na mwenendo wa makosa ya jinai (sura 20) ambapo jamhuri imefaili kiapo cha kuzuia dhamana kutolewa .

Upande wa mashtaka umepewa na mahakama hiyo nafasi ya kufaili hati kinzani Septemba 16 mwaka huu ili Septemba 18 mwaka huu maombi ya kutolewa ama kutotolewa kwa dhamana yatajulikana.

Wakili wa mwanahabari huyo Emmanuel Chengula kutoka mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) alisema kuwa hatua ya kufikishwa mahakamani kwa mteja wake ni mwanzo wa haki yake kupatikana kwani polisi walikuwa wakimzuia mahabusu mteja wao tangu  Jumamosi iliyopita bila kumpeleka mahakamani.

Wakili Chengula alisema katika kesi hiyo kuna maombi ya kuzuia dhamana ambayo ni maombi namba 10/2019 na kesi yenyewe ya msingi ni kesi namba 208/2019.

Mshitakiwa huyo amepelekwa katika mahabusu ya Isupilo Mufindi hadi septemba 18 atakapofikishwa mahakamani hapo tena kwa ajili ya kusikiliza maamuzi ya dhamana yake.
Na Francis Godwin - Iringa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527