TANZANIA YASAINI MKATABA WA KUPINGA MATUMIZI YA NYUKLIA.....YAPONGEZWA KWA KULINDA AMANI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Tanzania imesaini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia, na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 60 zilizosaini na 32 zilizoridhia mkataba huo Duniani.


Utiaji saini wa mkataba huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nchini Marekani.

Profesa Kabudi amesema kwa kusaini mkataba huo Tanzania inaunga mkono jitihada zote za kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia, ikiwa ni sehemu ya kuufanya ulimwengu kuwa mahali salama pa kuishi.


Hata hivyo Prof. Kabudi amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikatai na inaunga mkono matumizi ya amani ya nguvu za nyuklia kama sehemu ya dawa, kuhifadhi vyakula na uzalishaji wa nishati miongoni mwa matumizi mengine chini ya uangalizi madhubuti wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki.

Ameongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua hiyo ikitiliwa maanani kuwa zipo nchi zenye silaha za nyuklia takribani 14 elfu na zimetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuimarisha silaha hizo na kutoa wito kwa mataifa hayo kujenga imani kwa mataifa mengine na kwamba matumizi ya silaha hizo si njia sahihi na salama za kuihakikishia dunia amani na usalama. 



Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa umeipongeza  Tanzania kwa mchango wake wa kulinda amani katika ukanda wa maziwa makuu na kuahidi kushirikiana na Tanzania katika kuzuia matukio yanayosababishwa na misimamo mikali.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Plamagamba John Kabudi ambapo pia katika mazungumzo hayo wamegusia masuala ya maendeleo katika ukanda wa maziwa makuu, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa ya Burundi na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema umoja huo unatambua mchango na jitihada za Tanzania na kuongeza kuwa Umoja huo upo tayari kushirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kuzuia matukio yanayosababishwa na misimamo mikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527