SIMBACHAWENE AAGIZA TAASISI ZIANDAE MAZOEZI YA UPANDAJI MITI ZINAPOFANYA HAFLA MBALIMBALI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. George Simbachawene ameagiza taasisi ziwe zinaandaa utaratibu wa upandaji miti wakati wa matukio au sherehe mbalimbali hatua itakayohakikisha utunzaji wa mazingira unafanyika kwa ufanisi.

Pia amezitaka taasisi za umma, binafsi na za dini kuhakikisha zinaandaa vitalu vya miche ya miti na kugawa kwa wananchi waende kupanda akisema kuwa utaratibu huo utasaidia katika kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la miti nchini.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Pwaga wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe Mkoani Dodoma, Mhe. Simbachawene alisema wastani wa ukataji miti kwa mwaka ni 496,000 ambao unatokana na shughuli za kibinadamu, hali inayochangia uharibifu wa mazingira na kwa hali hiyo jukumu la kupanda miti ni la kila mtu.

“Nitafurahi kuona kiongozi yeyote anapofanya ziara mahali popote anaandaliwa utaratibu wa kupanda miti halafu ndio ahutubie mkutano na kwa kufanya hivyo tutaweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kukosekana kwa miti na hapa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inasema kila mtu ni taasisi ya mazingira hivyo ni lazima apande mti,” alisisitiza Waziri.

Kwa hali hiyo Mhe. Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe alitahadharisha kuwa matumizi ya mkaa kwa kiasi kikubwa yanachangia upotevu wa misitu yetu kwani unahusisha ukataji wa miti ya asili ambayo huleta mvua na uaoto wa asili.

Aidha, katika ziara hiyo Kijijini hapo pamoja na mambo mengine mara baada ya kuwasili Waziri huyo aliongoza zoezi la upandaji miti kwenye eneo la Kituo kipya cha Afya cha Pwaga kwa pamoja na viongozi mbalimbali Wilayani humo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Paul Sweya.

Waziri huyo alibainisha kuwa shughuli za kibinadamu ni nyingi na harakati za kutafuta maisha zinazosababisha akate miti kwa wingi zimeongezeka na hivyo kumfanya aharibu mazingira kwa kukata miti hivyo ni lazima sasa tulinde misitu yetu kwani ndio uhai wetu.

Kutokana na hilo aliwataka wananchi kuacha mara moja kuvichezea vyanzo vya maji huku na kutaka uwekwe msukumo zaidi kwa wananchi kuhusu suala zima la utunzaji mazingira na kuwa elimu itolewe kuanza ngazi ya shule za msingi ili wanafunzi wapate uelewa.

“Miti ni muhimu sana kwani kusaidia kupunguza mabadiliko ya tabianchi tena wataalamu wanasema ni vizuri kupanda miti ya asili kwani ina uwezo mkubwa wa kunyonya hewa ya kaboni ambayo ikiungana inatengeneza gesi joto ambayo inasababisha tabaka la ozone linalosababisha joto kubwa duniani,” aliasa Mhe.Waziri.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527