SERIKALI YAONYA MIFUGO KUTOKA NJE YA NCHI KUINGIZWA NCHINI KWA AJILI YA MALISHO | MALUNDE 1 BLOG

Friday, September 20, 2019

SERIKALI YAONYA MIFUGO KUTOKA NJE YA NCHI KUINGIZWA NCHINI KWA AJILI YA MALISHO

  Malunde       Friday, September 20, 2019

Serikali imewaonya wafugaji wanaoishi katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani kutoingiza mifugo ya raia wa nchi za jirani hapa nchini kwa ajili ya malisho na kuiweka katika vitalu walivyopewa kwenye ranchi za taifa na kutoa taarifa za uongo kuwa mifugo hiyo ni yao kwa kuwa atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo katika Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ambapo amebaini baadhi ya wafugaji wamekuwa wakikiuka sheria za nchi kwa kuchukua mifugo ya wafugaji wengine kutoka katika nchi za jirani na kuiweka kwenye ranchi hizo kwa ajili ya malisho ilhali wafugaji wengi nchini bado wanahitaji maeneo ya kulishia mifugo yao.

“Kwanza hairuhusiwi ng’ombe kutoka nje ya mipaka yetu kuingia nchini kuvuna majani na malisho ya hapa ndani ya nchi yetu kwa sababu sisi wenyewe tuna migogoro ya wakulima na wafugaji wetu ambayo hatujaimaliza na moja ya mikakati ni kuamua kutoa vitalu ili wafugaji wa Tanzania waweze kulisha mifugo yao atakayebainika kutofuata sheria za nchi atachukuliwa hatua za kisheria.” amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amesema mikakati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha Tanzania inaondokana na vikwazo vyovyote vilivyopo katika baadhi ya nchi kutonunua nyama kutoka hapa nchini kutokana na sababu zisizo sahihi kuwa mifugo ya Tanzania ina maradhi.

Kwa upande wake Meneja wa Ranchi ya Missenyi Bw. Oscar Mengele amesema ng’ombe waliopo katika ranchi hiyo wana afya njema na wamekuwa wakipatiwa dawa na kinga dhidi ya maradhi mbalimbali hivyo kuwa katika hadhi ya soko la kimataifa na kuwaasa wananchi kutangaza vyema nje ya nchi bidhaa zitokazo hapa nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa katika Ranchi ya Missenyi Mkoani Kagera katika ziara yake ya kikazi mkoani humo amepata fursa ya kuzungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu vilivyopo katika Ranchi ya Missenyi na kumuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Ugani na Mafunzo kutoka katika wizara hiyo Dkt. Angello Mwilawa kuratibu zoezi la elimu ya ufugaji bora kwa wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi zote zilizopo hapa nchini pamoja na kutafuta teknolojia ya kisasa yenye gharama nafuu kwa ajili ya kuogeshea mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali ambayo wawekezaji hao wanaweza kununua.

Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano serikalini
     Wizara ya Mifugo na Uvuvi


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post