SERIKALI YA TANZANIA YALAANI VURUGU ZA AFRIKA KUSINI DHIDI YA WAGENI

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Tanzania inaungana na Serikali ya Afrika Kusini kulaani vikali vitendo vya ubaguzi na mashambulizi vinavyofanywa na raia wachache wa nchi hiyo dhidi ya raia wa nchi zingine za Afrika na kuziasa nchi zingine kutolipa kisasi kutokana na vitendo hivyo.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 100 kutoka Tanzania wanaokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo iliyofanyika  jana tarehe 4 Septemba 2019 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Kabudi amesema kuwa, vitendo vinavyofanywa na raia wachache wa Afrika Kusini vya kuwashambulia raia kutoka nchi zingine za Afrika na kuharibu mali zao vinasikitisha na kuivunjia heshima nchi hiyo. Hata hivyo, alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaunga mkono kauli ya Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa aliyoitoa hivi karibuni ya kukemea na kulaani vikali vitendo vinavyofanywa na raia hao wachache.

Aidha, ameongeza kuwa, vitendo hivyo  ambavyo vinatokana na raia hao wengi kukosa ajira, ardhi na pia kutopenda kujishughulisha havihalalishi watu wengine wakiwemo watanzania kulipa kisasi kwa namna yoyote ile.

“Ni jambo la kusikitisha lakini Serikali ya Afrika Kusini inalisimamia kikamilifu na sisi tupo tayari kushirikiana nao ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.Nawasihi Watanzania wenzangu tusilipize kisasi na tutaendelea kuwalinda raia wa Afrika Kusini waliopo Tanzania kwani tunaamini kuwa Afrika ni moja na waafrika ni ndugu zetu” alisema Prof. Kabudi.

Kadhalika, Prof. Kabudi alieleza kuwa hadi sasa hakuna taarifa kuhusu Mtanzania kuuawa, kujeruhiwa au kuharibiwa mali kutokana na vurugu hizo. Pia alisema kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa za uhakika kadri zinavyopatikana kutoka kwenye vyanzo vya uhakika ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Wakati huohuo, Mhe. Prof. Kabudi amewaaga wanafunzi 44 kati ya 100 waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Wanafunzi hao ambao wengi wamehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Kilimo ya Uyole ya Mbeya na Ukiriguru ya Mwanza wanakwenda kushiriki mafunzo hayo ya vitendo kwenye sekta mbalimbali za kilimo ikiwemo uzalishaji na teknolojia. Kati ya Wanafunzi hao, 16 wameondoka nchini tarehe 4 Septemba, 2019, kuelekea Israel, 44 wataondoka nchini tarehe 5 Septemba 2019 na idadi iliyosalia itaondoka tarehe 10 Septemba 2019.

Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi amewataka wanafunzi hao vijana kuzingatia mafunzo hayo ili kuja kutoa mchango wao kwenye mapinduzi ya kilimo ambayo yatachochea mapinduzi ya viwanda nchini. Aidha aliwaasa kuwa waadilifu, kufanyakazi kwa bidii, kushikamana na kujiepusha na vitendo viovu.

“Mnaenda Israel kutafuta ujuzi, uzoefu na ubunifu katika maeneo ya uzalishaji mazao. Hivyo tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya kuja kuibadilisha Tanzania katika eneo la kilimo na mtaleta mapinduzi ya kilimo kwani vijana mpo wengi nchini, mna ari na ni nguvu kazi ya Taifa” alisisitiza Prof. Kabudi.

Akiielezea Israel, Mhe.Prof. Kabudi amesema kuwa nchi hiyo ni nusu jangwa kama ilivyo baadhi ya mikoa hapa nchini. Hata hivyo Israel inaongoza kwa kuuza mazao ya mbogamboga na matunda kwenye nchi za Ulaya kutokana na watu wa nchi hiyo kutumia maarifa katika kugeuza ukame kuwa fursa. Hivyo aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanapata maarifa na kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa ili kuja kuendeleza kilimo kikiwemo kile cha umwagiliaji kwenye mikoa kama Singida, Manyara, Shinyanga na Dodoma.

Wanafunzi hao mia moja (100) wamechaguliwa kati ya wanafunzi 1,440 waliotuma maombi ya kwenda kushiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel ambayo hufanyika kwa kipindi cha miezi tisa. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliratibu zoezi la upatikanaji wa wanafunzi hao kwa maelekezo ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwezi Novemba 2018 alipofanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini, Mhe. Noah Gal Gendler.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam.
4 Septemba 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527