RC MAKONDA AKABIDHI MUSWAADA WA MAPENDEKEZO YA SHERIA YA MIRATHI WIZARANI DODOMA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda  September 03 ametimiza ndoto za Wajane kwa kukabidhi Muswada wa Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Mirathi kwa Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwaajili ya Kufanyiwa maboresho na kufikishwa Bungeni.

 
Akikabidhi Muswada huo jana  Mjini Dodoma RC Makonda amesema ndani ya Muswada huo ameainisha mapendekezo ya kubadilishwa kwa Sheria kandamizi ambazo zimekuwa mwiba na Mateso kwa Wajane kwa muda wa miaka mingi.

Aidha RC Makonda amesema Miongoni mwa Sheria kandamizi anazopendekeza zifanyiwe mabadiliko ni Sheria ya Kiserikali ya Mirathi ya Mwaka 1865, Sheria ya Mirathi ya Kimila ya Mwaka 1963 na Sheria ya Mirathi ya Kidini ya Mwaka 1963 kwakuwa zimepitwa na Wakati na zimekuwa na Mapungufu mengi ya Kisheria.

RC Makonda amevitaja baadhi ya vipengele anavyopendekeza vifanyiwe maboresho ni pamoja na kipengele cha kumpa uhalali Mke wa marehemu kushiriki katika vikao vya mgawanyo wa mali, mjane kupewa haki ya kurithi na kusimamia mali za marehemu, Mjane kutoondolewa kwenye nyumba wala Mali kuhamishwa, Usawa wa watoto katika kumiliki mali za marehemu bila kujali jinsia pamoja haki ya mtoto wa nje ya Ndoa kurithi Mali.

Vifungu vingine ambavyo RC Makonda ameeleza kuwa ni kandambizi kwa Mjane ni pamoja na kipengele kinachoruhusu Mjane kurithiwa na kile kinachomnyima Mwanamke haki ya kurithi ardhi ya ukoo. 

Pamoja na hayo RC Makonda amesema chimbuko la muswada huo ni mapendekezo yaliyotokana na Kongamano la Wajane zaidi ya 5,181 alilohitisha mwezi April Ukumbi wa Mlimani City ambapo katika kongamano hilo alipokea Kero na Malalamiko yaliyomlazimu kuunda kamati iliyoshirikisha Wadau na Wataalamu mbalimbali kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa alichokifanya RC Makonda kupigania haki za wajane ni Ushujaa wa hali ya Juu na ameweka historia ya Jambo ambalo halijawahi kufanyika ambapo amemuahidi kufanyia maboresho ya haraka na kuwasilisha Bungeni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post