MTIHANI WA DARASA LA SABA 2019 KUANZA KESHO...WAKUU WA SHULE WAONYWA


Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania ( NECTA), Dkt. Charles Msonde akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufanyika kwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 unaotarajiwa kuanza kesho Septemba 11 na kumalizima Septemba 12 mwaka huu.

Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema vituo nane vilivyofungiwa mwaka jana baada ya kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba vitaendelea kutumia vituo mbadala vilivyopangiwa hadi baraza hilo litakapojiridhisha kuendelea kutumia vituo hivyo.

Katika mwaka huu 2019, watahiniwa 947,221 wamesajiliwa kufanya mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) unaotarajiwa kuanza kesho (Septemba11 na 12 mwaka huu) huku wakuu wa shule zote nchini wakipewa onyo kutojihusisha na udanganyifu wa mitihani hiyo.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde ameyasema hayo leo Septemba 10,2019 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema mwaka jana baraza ilifuta matokeo ya Shule za Msingi zote za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, Shule za Msingi Hazina, New Hazina (Kinondoni), Aniny Nndumi, Fountain of Joy (Ubungo), Alliance, New Alliance na Shule ya Msingi Kisiwani zote za Mwanza Jiji) na Shule ya Msingi Kondoa integrity (halmashauri mji wa Kondoa) kwa kufanya udanganyifu.

Amesema shule hizo zilifungiwa kufanyiwa au kusimamia mitahani zitaendelea kupangiwa vituo mbadala ambavyo vitaendelea kutumiwa na watahiniwa wanaoanza mtihani leo.

Aidha, Dk. Msonde amevitaja vituo vitakavyotumiwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa ni shule ya Hazina na New Hazina itatumia Shule ya Msingi Oysterbay, Shule ya Fountain of Joy na Aniny Nndumi zitatumia Shule ya Msingi Mbezi, mkoani Mwanza, Shule ya Kisiwani itatumia Kituo cha Shule ya Msingi Kakebe, Shule ya Msingi Alliance na New Alliance za Halmashauri Kondoa Mji mkoani Dodoma kituo kitakuwa Shule ya Msingi Mahina.

Dk. Msonde amesema kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa 451,235 ambao ni sawa na asilimia 47.64 ni wavulana na watahiniwa 495,986 ambao no sawa na asilimia 52.36. Waliosajiliwa ni wasichana na kuongeza kuwa kati ya hao, watahiniwa 902,262 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili na watahiniwa 44,959 watafanya mtihani kwa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia kujifunzia ambapo mtihani huo utakuwa na masomo ya Kiswahili, English Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

Pia ametaja watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 2,678 kati yao 81 ni wasioona, 780 wenye uoni hafifu, 628 wenye ulemavu wa kusikia, 325 ni wenye ulemavu wa akili na 864 ni wenye ulemavu wa viungo," amesema Dk Msonde.

Dk. Msinde pia ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa Halmashauri na Majiji kuhakikisha kuwa taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa zinazingatiwa kwa kuhakikisha mazingira ya vituo kuwa salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu na wasimamizi wot walioteuliwa wameaswa kufanya kazi kwa umakini na uadilifu kulingana ja kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa.

"Baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha au kusababisha udanganyifu wa mitihani kufanyika kwa kujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma. Tunaomba wadau kutoa taarifa katika vyombo husika kila mnapobaini uwepo wa mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani wa aina yoyote ile," amesema Dk Msonde.

Baraza hilo limewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi cha kufanyika mtihani huo kwani hawatasita kufuta kituo chochote endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani hiyo.

pia wasimamizi, wametakiwa kuhakikisha wanalinda haki za watahiniwa wenye mahitaji maalum kwa kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527