MKUU WA MAJESHI NCHINI JENERALI MABEYO ACHANGISHA ZAIDI YA MILIONI 40 KUJENGA NYUMBA YA MAPADRE JIMBONI RULENGE NGARA

Na Avitus Benedicto Kyaruzi, Kagera

Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo ameshiriki na kuendesha harambee ya ujenzi wa nyumba ya  Mapadre wa Parokia ya Mtakatifu Francisco wa Assiz Jimbo Katoriki la Rulenge Ngara  Mkoani Kagera ambapo pamoja na kuchangia ujenzi huo lakini pia aliwaongoza na kuwahamasisha waamini wa jimbo hilo kuchangia ujenzi huo.


Akiwakilishwa na Lt.  Jenerali Mnadhimu Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania Samwel Ndomba katika harambee hiyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi za Baba Askofu wa Jimbo Katoriki la Rulenge Ngara Seveline Niwemugizi Septemba 8, 2019 Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo alichangia kiasi cha shilingi milioni kumi na kuchangisha jumla ya shilingi milioni arobaini taslimu na ahadi katika harambee hiyo. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akimuunga mkono Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Mabeyo katika harambee hiyo alichangia shilingi milioni kumi taslimu na kusema kuwa nyumba hiyo si ya Mapadre tu bali ya viongozi mbalimbali wa nchi ambao wanaweza kusema neno kwa wananchi  na mkoa ukasonga mbele kwa maendeleo hasa kwa kupunguza mauaji katika jamii.

Awali kabla ya harambee hiyo mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi nchini Lt. Jenerali Mstaafu Ndomba alishiriki katika ibada takatifu iliyongozwa na Askofu wa Jimbo Katoriki la Rulenge Ngara Seveline Niwemugizi katika Parokia ya Mtakatifu  Francisco wa Assiz Ngara ambapo aliweza kutoa ujumbe kwa waamini wa kanisa hilo kuchangia ujenzi wa nyumba za Mapadre katika Parokia hiyo.

Luteni Jenerali Mstaafu Ndomba ndani ya Kanisa aliwakumbusha waamini kuwa ni heri kumtolea Mwenyezi Mungu mchango kabla yeye mwenyewe hajaamua kujichukulia. 

“Baadhi ya waamini hujifikiria mara mbili kutoa michango au hutoa chenji badala ya kutoa kitu kizima lakini hewa safi tuvuta bure wote hapa wakati kuna wagonjwa hospitalini wanaivuta kwa kulipia  gharama kubwa na hili ni angalizo kwetu kutoa michango kujenga kanisa la bwana.” Alisisitiza Lt. Jenerali Mstaafu Ndomba.

Luteni. Jenerali Mstaafu Ndomba alitolea mfano wa Makanisa ya Ulaya kuwa kwasasa makanisa hayo wamebakia waamini wazee tu vijana hawaendi tena kanisani na wakati huo huo Afrika Makanisa yanazidi kujaa waamini na sababu kubwa ni Makanisa hayo kutoa huduma mbalimbali za kiroho na kijamii kama elimu na afya na kuwagusa vijana walio wengi na kuamua kumfuata Kristo.

Naye Askofu Seveline Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara akiongoza ibada hiyo ya harambee aliwakumbusha waamini kuwa wafuasi halisi wa Kristo na wasiwe mashabiki tu ambao hupenda kusikiliza mtu anaongea nini na kuishia hapo,  bali wabebe msalaba wa kweli kwa kushiriki na kuchangia michango mbalimbali kama wanafunzi wa Yesu walivyojitoa na kuwa wafuasi wa kweli na si mashabiki.

“Tumekuwa tukieneza injili na kuombea miito na vijana wameitikia wito kweli kweli, hivi juzi tulikuwa katika kikao cha bodi ya Seminari zetu kuu tano nchini ambazo ni Segerea, Kipalapala, Ntungamo, Kibosho na Peramiho vijana wetu sasa hawana pa kukaa, sasa sisi waamini lazima tubebe msalaba wa kuwapatia mahala pa kuishi kwa kuchangia ujenzi wa nyumba mpya au upanuzi wa zilizopo.” Alisisitiza juu ya michango Askofu Niwemugizi.

Naye Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Francisco wa Assiz Ngara Padre Sixmund Nyabenda aliwakumbusha waamini kuwa wamisionari waliokuwa wakitoa michango ya ujenzi wa kanisa la Mungu hawapo tena na kama wapo huko nchi za Ulaya wapo katika vyumba vya wagonjwa mahututi na akasema wamisionari ni waamini wenyewe wa kujenga kanisa la Mungu.

Ujenzi wa nyumba ya Mapadre Parokia ya Mtakatifu Francisco wa Assiz Ngara unahitaji kiasi cha shilingi milioni 400 na inatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Aidha, katika harambee hiyo mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi nchini Lt. Jenerali Mstaafu Ndomba aliweza kuchangisha zaidi ya shilingi milioni 30 taslimu na ahadi zaidi ya shilingi milioni 10.5 ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi ambavyo ni saruji mifuko 95.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post