KATIBU WA WAZAZI CCM KAGERA AWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KUFICHUA WANAOTIA MIMBA WATOTO


Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Kagera, Angelus Wilbard Kamugisha

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Wananchi wametakiwa kukemea na kutoa taarifa wanapoona au kuhisi kuwepo kwa vitendo vya baadhi ya watu kuwapa mimba watoto na kusababisha kukatisha masomo na ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 6, 2019 na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Kagera, Angelus Wilbard Kamugisha wakati akiongea na vyombo vya habari katika ofisi za chama cha mapinduzi (CCM) zilizopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Kamugisha ametaka wazazi walezi na wananchi kwa ujumla kukemea tatizo la mimba za utotoni zinazosababisha kukatisha masomo na ndoto zao ametaja vitendo hivyo kuwa kero licha ya kupigiwa kelele kila mara na baadhi ya viongozi.

Amesema elimu bure imetolewa hapa nchini kwa ajili ya kumpatia uelewa mtoto lakini baadhi ya watu wasiojua misingi,sheria na kanuni za nchi wameendelea kukiuka utaratibu katika kufanya vitendo hivyo ambavyo unalifedhehesha taifa kutokana na kuwakosa wategemewa wa baadae.

"Watoto hukatishwa masomo, hukaa majumbani kwa sababu ya kupewa ujauzito huku wengine wakiwa bado katika umri mdogo. Changamoto kubwa iliyopo ni wazazi kutotoa ushirikiano wa kutoa taarifa sahihi pale binti anapata ujauzito matokeo yake inamuathiri kisaikolojia huyo binti,"amesema.

Amewataka vijana kuachana na makundi mabovu yanayosababisha mmomonyoko wa maadili, huku akiwataja waendesha pikipiki kuwa chanzo cha kuharibu watoto wa shule na kuwataka kuacha tabia hizo mara moja.

Amesema waendesha pikipiki wameeongelewa sana katika baadhi ya sehemu tofauti kuwa ni kikwazo kwa kuwarubuni watoto wa shule kwa rifti zinazojenga vishawishi vya kuwapa mimba wanafunzi  hivyo ametaka kuacha tabia hiyo mara moja.

Amesema juhudi kubwa za serikali ni kuwa na mpango wa kuhimiza kujengwa kwa mabweni shuleni ili kuepukana na watoto wa kike kutembea umbali mrefu ambapo tayari kila kata ina shule ikilinganishwa na awali.

Hata hivyo amesema katika baraza la Jumuiya ya wazazi la mkoa limetolewa azimio kuwa kila wilaya iunde kamati ya kutoa elimu juu ya maadili mema kwa vijana walioko mashuleni na mitaani, kufuatilia afya na mazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527