RAIS MAGUFULI AMTAJA TUNDU LISSU...ASEMA ALITELEKEZA JIMBO LAKE


 Rais wa Tanzania, John Magufuli amempongeza mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu akisema jimbo hilo lilikuwa limetelekezwa na Tundu Lissu.


Mtaturu amechaguliwa hivi karibuni kuwa mbunge wa Singida Mashariki kuchukua nafasi ya Lissu ambaye Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alitangaza kuwa amepoteza sifa za kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza leo Jumatatu Septemba 16, 2019 katika hafla ya uzinduzi wa rada za kuongoza ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Rais Magufuli amewapongeza wajumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu pamoja na mbunge huyo wa Singida Mashariki, aliyemtaka akawatetee wananchi bila kujali vyama.

“Nimefurahi kumuona hapa kwenye Kamati ya Miundombinu mbunge wa CUF (hakumtaja jina), lakini pia na mheshimiwa nani yule wa lililokuwa jimbo lililokuwa limetelekezwa. Ni jimbo gani hili.”

Huku akikuna kichwa Magufuli amesema, “Lilikuwa la Tundu Lissu ameshika huyu (huku akimnyooshea kidole Mtaturu).”

Ameongeza, “Safi kabisa hongereni mpigie makofi na ameingia na kazi nakuahidi Serikali yangu tutashughulikia maji katika jimbo hilo.”
Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527