CHAMA CHA MAPINDUZI CCM CHAZINDUA RASMI GAZETI LA UHURU YA KIJANI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

CHAMA cha Mapinduzi(CCM), kimewataka wenyeviti wa mashina na mabalozi kutopanga foleni wanapofika kwenye ofisi za  serikali.

Kauli hiyo aliitolewa leo  jijini hapa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Taifa, Dk. Bashiru Ally,  wakati wa  uzindua wa gazeti la ‘Uhuru ya kijani’ ambalo linalenga kujenga na kuimarisha chama hicho.

Alisema kuwa mabalozi hawana kizuizi hata kwenye kugombea wao hawaitwi na hawazuiliwi wanaweza kugombea hata urais.

“Mwenyekiti wa shina au balozi akipiga simu au kupiga hodi sehemu yeyote zilipo ofisi za viongozi wa serikali naomba asipange foleni,”alisema.

Aidha, Dk. Bashiru alieleza kuwa, wamepanga kuwapatia vitambulisho  viongozi hao kwa sababu ndio njia pekee ya kutambua mchango wao kwa kuwa, viongozi hao katika ngazi ya chini ya chama wamekuwa wakijitolea Zaidi kuliko wanachama wengine.

“Chama chetu kitaendelezwa kwa njia ya kujitolea na nitumie fursa hii wabunge wetu na wabunge wa baraza la wawakilishi mfanye  kazi kwa kujitolea ili kuimarisha chama chetu,”alisema.

Dk.Bashiru alisema kazi wanayoifanya ni kuwalinda wabunge dhidi ya  wanaowasumbua na watu wasiofuata taratibu hivyo nao wasaidie kuimarisha chama.

Akizungumzia mkakati wa Umoja wa Vijana wa CCM(UVCCM) wa ‘Tanzania ya kijani’, Dk.Bashiru alisema mkakati huo umepokelewa vizuri na kuwataka usitumike kama makongamano ya kuonekana kwenye TV na mitandao ya kijamii ikiwemo ‘You tube’

“Sasa nataka vijana wabadilike kutoka kwenye hamasa waende kwenye kazi ya siasa ya kuimarisha chama ili shughuli ipimike, vinginevyo huu mkakati nitausimamisha nimeshaongea na katibu ni mkakati mzuri tusiposimamia unaweza kuzaa jambo ambalo hatujalitarajia,”alisema.

Alieleza kuwa vijana wawe na mvuto wa kukilinda chama na inapotokea mtu anakichokoza chama ahame chama aonekane ni jasiri na sio legelege.

Kuhusu gazeti hilo, Dk.Bashiru alisema litatumika kujenga na kuimarisha chama nayeye atakuwa na ukurasa wake ambao atakuwa anazungumzia kuhusu urithi.

Alisema katika ukurasa huo kutakuwa na mambo matano ikiwemo haki, tunu za taifa.

“Kuna mjadala kuhusu tunu za Taifa kulikuwa na mjadala hata kwenye Bunge la Katiba ambapo moja ya tunu ni lugha ya Kiswahili, na gazeti hili litatumika kukuza Kiswahili,”alisema.

Alisema kati ya mambo ambayo yamefanyika chini ya uongozi wa Spika Job Ndugai ambayo ni kubwa kuliko yote ni uamuzi wa kimapinduzi wa kulinda rasilimali kwa kutunga sheria ambayo inaonesha nchi imegoma kugeuzwa shamba la bibi.

Aidha alisema katika mikakati ya kisiasa ya kuimarisha uhai wa chama ipo minne ambapo ni pamoja na kukomaza demokrasia mashinani kupitia kwa wenyeviti wa mashina na mabalozi ili kukifanya kuwa karibu na wananchi na wanachama.

Awali, Spika wa Bunge Job Ndugai, alipongeza kuanzishwa kwa gazeti hilo na kudai kuwa kukosekana kwa habari kwenye matawi kumekuwa ni unyonge mkubwa.

“Gazeti lina habari za kuelimisha jambo hili ni jema nakuahidi sisi wabunge tutatoa kila aina ya ushirikiano, tutachukua nakala kwa idadi ya matawi, kata, na wilaya na limekuja wakati muafaka maana tunaelekea kwenye uchaguzi,”alisema.

Alisema chama kina nguvu kubwa ya kuvitumia vyombo vyake vya habari ili kukabiliana  na vitendo vya upotoshaji.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post