BITEKO: TUME YA MADINI ANDAENI UTARATIBU BIASHARA YA MADINI IFANYIKE KIKANDA

Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Waziri wa Madini Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuandaa haraka utaratibu utakaowawezesha Wafanyabiashara wa Madini nchini kufanya shughuli zao katika ngazi ya Kanda tofauti na ilivyo sasa ambapo taratibu zinawataka kufanya shughuli hizo katika Mikoa zilipotolewa leseni zao.

 
Aliyasema hayo Septemba 7, 2019 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao na wizara uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na  Viongozi na Wataalam wa wizara na Taasisi zilizo chini yake.

Aidha, Waziri Biteko alieleza kuwa, endapo wadau hao watafanya shughuli zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa, serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutanua wigo kuwawezesha kufanya biashara ya madini katika maeneo mengi zaidi.

Waziri Biteko alisisitiza kuhusu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya kutaka rasilimali madini kulinufaisha taifa na watanzania  na kueleza kuwa, ndoto hiyo ndiyo iliyopelekea  kufanyika kwa mageuzi mkubwa katika Sekta ya Madini.

Alikiri kuwa, kabla ya mabadiliko hakukuwa na mfumo rasmi uliowaonesha wachimbaji kujua sehemu sahihi ya kuuzia madini yao vivyo hivyo kwa wanunuzi wa madini suala ambalo lilipelekea kuwepo vitendo vya utoroshaji madini jambo ambalo lilionekana ni la kawaida.

Waziri  Biteko aliwataka wafanyabishara hao kuyatumia masoko yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini  na kusisitiza  kuwa, serikali itaendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini na kueleza kuwa, waliobainika kufanya vitendo hivyo wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na hivyo kuwataka kuwa  chanzo  cha mabadiliko ili kuzuia vitendo vya utoroshaji madini.

‘’ Tumekutana mpaka na wakemia wanaotengeneza madini feki. Kuna wengine wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunataka chumba cha madini kiwe na hewa ya kutosha,’’ alisisitiza Biteko.

Akijibu hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabishara wa Madini ya Vito (TAMIDA) Sam Mollel, kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, Waziri Biteko aliwataka kuwa na subira wakati serikali  ikishughulikia suala hilo.

Aidha, akijibu  changamoto  ya Masonara kusimamiwa  na  wizara nyingine, Waziri Biteko  aliwataka wafayabiashara hao kuwasilisha maoni kuhusu suala hilo  kama ilivyofanyika katika kuandaa Kanuni za Masoko na kuongeza kwamba,   ‘’ Tunataka kuwa wizara ambayo inatatua matatizo’’.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisisitiza kuhusu suala la kulipa kodi kama inavyowapasa na kuwataka kuyafahamu mabadiliko yaliyofanywa katika sekta na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, aliipongeza wizara kwa kazi ya kuwalea wadau wa madini na kueleza kwamba, miaka ya nyuma mambo kwenye sekta hayakuwa yakienda vizuri. 

Aidha, aliwapongeza wafanyabiashara wa madini na kueleza kuwa, hivi sasa wameanza kubadilika huku tabia ya kufanya biashara ya madini kiholela ikianza kutoweka.

‘’ Sisi Kamati tunapoona mambo yanakwenda vizuri mnaturahisishia kazi yetu’’, alisisitiza Mwenyekiti wa Kamati. 

Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni jitihada za wizara  za kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini  ikiwemo kusikiliza na kutatua  changamoto kwenye sekta  ili kuwezesha biashara ya madini kufanyika katika mazingira mazuri yanayoleta tija kwa pande zote. 

Aidha, sambamba na mkutano huo, imefanyika Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kubwa ikiwa ni serikali kueleza nia yake ya kukifanya Chuo Cha Madini Dodoma kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Akifunga semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula alitaka mchakato wa wa kukilea Chuo hicho kutochukua muda mrefu na alikitaka kijisimamie chenyewe ndani ya muda mfupi baada ya kulelewa  na kutoa elimu bora.

Pia, alitaka kozi ya Mafundi Mchundo kuwekewa msingi mzuri.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti wa Kamati aliitaka wizara kukiongezea nguvu Kituo Cha Jimolojia Tanzania (TGC) ikiwemo bajeti ya kutosha kukiwezesha kuboresha miundombinu yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527