ALICHOKISEMA TUNDU LISSU BAADA YA MAHAKAMA KUU KUTUPILIA MBALI KESI YAKE


Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema atakata rufaa kupinga Mahakama Kuu kukataa maombi yake ya kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.



Jana, Jaji Sirillius Matupa alisoma uamuzi kuhusu maombi ya Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, akibainisha kuwa  hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Jaji huyo alisema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Kupitia mitandao ya kijamii, Lissu amesema amewasiliana na wakili wake, Peter Kibatala kuhusu uamuzi huo akidai  unaoonyesha kuwa mahakama ina hofu.

"Sisi hatukuwa, na bado hatuna, ugomvi na Tume ya Uchaguzi wala na Miraji Mtaturu. Ukifungua kesi ya uchaguzi, kama anavyoshauri Jaji Matupa, unatakiwa kuthibitisha kwamba una ’cause of action’, i.e. ugomvi na aliyechaguliwa au aliyesimamia uchaguzi.

"Tume iliitisha uchaguzi kwa sababu iliandikiwa barua na Spika Ndugai kwamba kiti cha ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kiko wazi. Haijatukosea sisi na, kwa sababu hiyo, hatuwezi kuishtaki kwa njia ya kesi ya uchaguzi.

"Miraji Mtaturu aligombea uchaguzi na kutangazwa ‘mshindi’ kwa sababu aliitikia wito wa Tume. Hajatukosea sisi na, kwa sababu hiyo, hatuwezi kumshtaki kwa kutumia njia ya kesi ya uchaguzi.

"Aliyetukosea ni Spika Ndugai; na ‘dawa’ stahiki kwa makosa yake sio kesi ya uchaguzi, bali ni marejeo ya kimahakama ya uamuzi wake. Hatukukosea chochote kufungua maombi ya marejeo ya kimahakama.

"Hoja ya kwamba kutakuwa na mgogoro wa kikatiba, wabunge wawili, etc., ni hoja isiyokuwa na mantiki au maana yoyote.

"Tulichoomba sisi ni Mahakama Kuu itamke kama uamuzi wa Spika Ndugai ulikuwa sahihi kisheria. Once Mahakama Kuu ikitamka kwamba uamuzi huo haukuwa sahihi kisheria, maana yake ni kwamba yote yaliyofanywa na Tume kufuatia uamuzi huo yalikuwa batili.

"Kama uamuzi wa Spika Ndugai ni batili maana yake ni kwamba uchaguzi ulikuwa batili na hakuna mbunge mpya aliyechaguliwa kihalali. Kwa hiyo hakuwezi kuwa na wabunge wawili kwenye nafasi moja. Tunakwenda Mahakama ya Rufaa ya Tanzania,”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527