WIZARA YA KILIMO YAJA NA MKAKATI WA TAIFA WA MIAKA 10 WA USIMAMIZI WA MAZAO BAADA YA KUVUNWA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji, teknolojia duni za kuhifadhi mazao baada ya mavuno, uelewa mdogo wa wadau katika kukabiliana na upotevu wa mazao na uhaba wa miundombinu ya masoko.


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yameanza leo tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Mhe Hasunga amesema kuwa wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo watapata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ya bidhaa za kilimo  ili kuona hali halisi ya Maadhimisho pamoja na teknolojia za uzalishaji,  uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, zilivyoandaliwa. Waoneshaji wengine wako njiani na tunatarajia uwanja huu wa Nyakabindi utafurika kwa maonesho.

Alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo za upotevu wa mazao baada ya kuvuna, Wizara ya Kilimo imetayarisha Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvunwa.

Alisema kuwa Mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na malengo endelevu ya dunia ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama wa chakula na lishe na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa Mataifa kati ya Malengo 17.

“Katika utafiti uliofanyika inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 watu watakuwa bilioni tisa (9) na hivyo mahitaji ya chakula yatakuwa asilimia 60 zaidi ya mahitaji ya sasa. Hivyo basi mkazo utakuwa kuzalisha chakula kati ya asilimia 50 – 70 zaidi ya sasa. Hivyo, udhibiti wa upotevu wa mazao ya chakula ni suala muhimu na la kipekee” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

Mkakati huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha, Mkakati huo umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.

Alisema, suala la udhibiti wa upotevu wa mazao ya chakula ni suala muhimu na la kipeee, linalopaswa kupewa kipaumbele na kila Mdau katika mnyororo wa thamani na shabaha yetu ni kupunguza upotevu kwa asilimia 50 ya mazao ya chakula ifikapo 2025.

Waziri Hasunga ametaja Mkakati huo kuwa una malengo makuu tisa ambayo ni Kujenga uelewa  kuhusu usimamizi wa mazao baada ya kuvuna ili kuboresha ufanisi na kupunguza upotevu wa mazao katika mnyororo wa thamani; Kuhamasisha upatikanaji, ufikiaji, unafuu na utumiaji wa teknolojia na mbinu zilizothibitishwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna; Kuwezesha mifumo ya masoko ya kilimo, ili kuboresha upatikanaji wa soko na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna; na Kuhamasisha tatifi na uvumbuzi wa teknolojia mpya inayoendana na mazingira yetu pamoja na mbinu za kupunguza upotevu wa mazao.

Mikakati mingine ni Kupitia na kuweka sheria mpya ili kuhakikisha kuwa viwango vya ubora vinazingatiwa kwa mujibu wa sheria ili kupunguza upotevu baada ya kuvuna; Kuimarisha uwezo wa taasisi, uratibu, ushirikiano, ubia na ushiriki wa Wadau wa usimamizi wa upotevu baada ya kuvuna katika kuimarisha utekelezaji malengo ya kimkakati; Kutengeneza mifumo ya usimamizi wa mazao  baada ya kuvuna ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi; Kukabiliana na upungufu wa fedha katika kugharamia usimamizi wa mazao baada ya kuvuna; na Kuwa na mbinu za kiwango kinachokubalika za kukusanya taarifa za upotevu wa mazao baada ya kuvuna nchini.

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine wameandaa mpango wa kutekeleza Mkakati huo. Ili kutekeleza mpango na malengo hayo kwa ufanisi ni vema kushirikikana Wadau wote kwenye mnyororo wa thamani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527