WAZIRI WA VIWANDA: SERIKALI IMEONDOA KODI KERO 54 KWA WAFANYABIASHARA

Na Amiri kilagalila-Njombe

Waziri wa viwanda na biashara Innocent Bashungwa amesema serikali imefuta kodi kero  54 kwa wafanyabiashara pamoja na kupunguza mamlaka za kutoa leseni za biashara.

Bashungwa ameyasema hayo mjini Makambako mkoani Njombe wakati akizungumza na wafanyabiashara kutoka mikoa zaidi ya 7 nchini waliokutana  mjini hapo kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya biashara na kuja na maazimio ya kuiomba serikali kupunguza utitili wa kodi,tozo na leseni kwa wafanyabiashara ili kunusuru sekta hiyo ambayo imetajwa kuwa katika hali mbaya kimaendeleo kwa sasa.

“Kuna kodi 54 zimeishaondolewa na ili nisiseme tu 54 mheshimiwa mwenyekiti wenu nimeisha mkabidhi hizo kodi kero 5”alisema Bashungwa

Awali wakizungumzia changamoto hizo wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka mikoa ya Tanga, Dar es salaamu,Mbeya,Songwe, Ruvuma, Iringa,Njombe na Katavi wamesema hali ya biashara nchini imezidi kuwa ngumu kwasababu kumekuwa na mrundikano wa tozo na ushuru kutoka mamlaka mbalimbali ikiwemo TRA,Halmashauri na nyinginezo hatua ambayo inawafanya watu wengi kufunga biashara zao.

Amani Mahellah,Sifael Msigala na Ismail Masoud ni baadhi ya wawakilishi walitoa maoni yao katika mkutano huo mkubwa wa wafanyabiashara nchini ambapo wamemuomba waziri wa viwanda na biashara Innocent Bashungwa kuhakikisha anakutana na wizara zote zinazomgusa mfanyabiashara katika majukumu yake ili kuzitafutia ufumbuzi changomoto hizo kwa ustawi wa sekta ya biashara na taifa kwa ujumla.

“Hizi taasisi zinazokusanya kodi za serikali zikutane kwa pamoja na wafanyabiashara ili kila mtu ajue kwa mfanya biashara yule anachukua shilingi ngapi”alisema Amani Mahellah mmoja wa wafanyabiashara

Akifafanua kiini cha kusuasua kwa sekta ya biashara nchini katibu mkuu wa jumuiya ya wafanyabiashara JWT Abdallah Mwinyi amesema kuwepo kwa urasimu mkubwa bandarini kunawafanya kutengeneza mianya ya rushwa huku  kamishna wa TRA nchini Edwin Mhede akimtaka kila mfanyabiashara kuviripoti vitendo vyote vya rushwa kwani vinaikosesha nchini Mapato.

“Forodha aangaliwe kwa makini nap engine sheria zibadilishwe kwenye udhaminishaji na uondoshaji mizigo bandalini” alisema Abdallah Mwinyi

Katika mkutano huo wizara nne zenye mahusiano ya karibu na wafanyabiashara zimealikwa ikiwemo ya viwanda na biashara ,tamisemi, fedha na uwekezaji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527