WAZIRI WA NISHATI DR. MEDARD KALEMANI ATOA UFAFANUZI KWA KAMATI YA BUNGE KUHUSU UUNGANISHWAJI UMEME KWA WATEJA WA VIJIJINI

Na Veronica Simba – Dodoma

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa idadi ya  wanaounganishiwa umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea ni ya awali na itakuwa ikiongezeka kadri wananchi husika watakavyokuwa wakilipia gharama yake ambayo ni shilingi 27,000 tu.

Alieleza hayo jana, Agosti 20, 2019 jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na wajumbe kadhaa wa Kamati hiyo walioonesha wasiwasi wao kuwa idadi ya wananchi wanaounganishiwa umeme vijijini ni ndogo.

“Kinachofanyika hivi sasa ni kupeleka miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali vijijini na kuunganisha wateja wa awali. Wengine wataendelea kuunganishwa kwa wakati wao kadri wanavyolipia,” alifafanua Waziri.

Aidha, kuhusu agizo la serikali kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kutumia vifaa vya ndani ya nchi, Waziri ameieleza Kamati husika kuwa msimamo huo unatokana na matumizi ya vifaa vya ndani kuwa na tija zaidi kuliko vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.

Akifafanua, alieleza kuwa kuagiza vifaa nje ya nchi ni gharama kubwa ukilinganisha na kutumia vifaa vya ndani. Pia, alisema, ni rahisi zaidi kwa serikali kusimamia na kudhibiti ubora wa vifaa vya ndani kuliko vinavyotengenezwa nje ya nchi. Vilevile, aliongeza kuwa muda unaotumika kupata vifaa vinavyotengenezwa ndani ya nchi tangu siku vinapoagizwa ni mdogo kulinganisha na ule unaotumika kuagiza na kuletewa vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Waziri pia alizungumzia katazo lililotolewa na serikali kuhusu wananchi vijijini kulipia nguzo ambapo alisema uamuzi huo ulifikiwa ili kuwapunguzia gharama wananchi hao ambao wengi kipato chao ni kidogo.

“Kwa uhalisia, umeme vijijini unatolewa bure kwa wananchi na gharama zake kuchukuliwa na serikali. Hata hiyo 27,000 wanayolipa ni gharama za ushuru wa thamani tu ambayo ni asilimia 18 ya gharama husika. Sasa ukimlipisha mwananchi huyo nguzo itarudisha tatizo palepale, hivyo nasisitiza tena kwamba wananchi wa vijijini hawatakiwi kulipia nguzo.”

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, ameieleza Kamati hiyo kuwa, tangu kuanzishwa kwake, REA imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Miradi ya Awali, Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Kwanza (REA I), Awamu ya Pili (REA II) na Awamu ya Tatu (REA III).

Amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo mwaka 2021, kutawezesha vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara kufikiwa na miundombinu ya umeme.

Katika kikao hicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilikuwa ikipokea taarifa ya maendeleo na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya REA pamoja na changamoto inazokabiliana nazo.

Wengine walioshiriki kikao hicho ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527