MANYANYA AWAONYA WANAOENEZA PROPAGANDA CHAFU NA KUKIMBIZA WAWEKEZAJI TANZANIA


Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog
Serikali imesema haikuwafumbia macho watanzania watakaojaribu kuikashfu nchi kwa maneno ya propaganda zinazosababisha kuwakatisha tamaa wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 16 2019, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Eng.Stella Manyanya akiwa mkoani Kagera katika hitimisho la wiki ya Uwekezaji Kagera iliyofanyika katika uwanja wa Gyamkana uliopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.


Manyanya alisema kuna baadhi ya watu wenye tabia ya kutoa maneno ya propaganda ya kuikashfu nchi ya Tanzania jambo linalokatisha tamaa wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuwekeza hapa nchini.

"Hatutokuwa tayari kuwakumbatia wanaokwamisha maendeleo, propaganda na maneno havina nafasi, serikali imejipanga kikamilifu na hatutamuonea huruma mtu yeyote anayetaka kujaribu kuichafua nchi hii iliyojawa amani na upendo",alisema.

"Watanzania tuache kuiuza nchi yetu kwa maneno ya Propaganda. Huu sio muda wa maneno maneno badala yake watu wajitathmini na kuona ni wapi wamefanikiwa na ni wapi wanakwama kibiashara kwa kukaa kwa pamoja na kujadiliana na kuinua uchumi wa mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla",aliongeza Manyanya.

Aliwataka wafanya biashara kuzingatia bidhaa bora huku akimpongeza Rais Magufuli kwa kuondoa utitiri wa kodi zilizokuwa zikikwamisha biashara nchini.

Aidha aliahidi ushirikiano na wana Kagera katika suala la kibiashara na kumpongeza mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti katika kubuni wiki ya uwekezaji Kagera kwani hadi sasa Kagera imenoga kwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527