HARUFU KALI YA USHUZI YAVUNJA KIKAO CHA BUNGE KENYA

Mjadala mkali juu ya hali ya masoko ulikatizwa ghafla kwa harufu kali ya ushuzi.

Kadhia hiyo haikutokea sokoni ama mtaani, bali ni kwenye ukumbi wa Bunge la Kaunti ya Homa Bay, Magharibi mwa Kenya.

"Mheshimiwa Spika, mmoja wetu hapa amechafua hali ya hewa," Bw Julius Gaya anaripotiwa kupiga ukelele akiwa kwenye kikao cha Bunge.

Lakini mjumbe aliyerushiwa lawama za kujamba alikanusha vikali akisema: "Sio mimi. Siwezi fanya kitendo kama hicho mbele ya wenzangu."

Katika jitihada za kupambana na harufu hiyo, Spika Edwin Kakach akaamuru wajumbe wote watoke nje kwa muda.

Ripoti pia zinaeleza kuwa aliagiza marashi "ili kuleta harufu nzuri. Lete (marashi) ya aina yeyote utakayoyakuta ofisini kwangu.

"Hatuwezi kuendelea kukaa kwenye mazingira ya kunuka."

Hata hivyo inadaiwa harufu hiyo ilikatika kabla ya marashi hayo kupatikana hali iliyoruhusu kikao kuendelea.

Inaripotiwa kuwa tukio hilo la kipekee lilitokea Jumatano wiki hii.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527