UCHUMI WA UKANDA WA KUSINI, WAVUTIA UFUGAJI WA KISASA | MALUNDE 1 BLOG

Monday, August 19, 2019

UCHUMI WA UKANDA WA KUSINI, WAVUTIA UFUGAJI WA KISASA

  Malunde       Monday, August 19, 2019
Na. Edward Kondela

Kutokana na watu wengi kuitikia wito wa serikali kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe bora wa maziwa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2019/20 imeweka mikakati ya kuliimarisha shamba lake la kuzalisha Mifugo la Nangaramo lililopo Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara ili kusogeza zaidi huduma hiyo kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea shamba la Nangaramo na kujionea mafanikio na changamoto zilizopo katika shamba hilo Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde amesema wizara imedhamiria kuhakikisha Shamba la Nangaramo linapata ng’ombe bora wa kisasa wa maziwa, ng’ombe wazazi pamoja na kumpeleka mtaalamu katika Kituo cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha kujifunza uhimilishaji ili aweze kutoa huduma katika shamba hilo.

“Shamba linatoa huduma katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma nia ya kuleta ng’ombe bora wa kisasa hususan kwa wafugaji ni kupata uzalishaji bora pamoja na wafugaji hao kufuga kisasa, Shamba la Nangaramo ni muhimu sana tutahakikisha mwaka huu wa fedha tunalisaidida ili liweze kutoa tija kwa wananchi kwa kuweza kununua ng’ombe bora na kisasa kutoka katika shamba hili.” Amesema Dkt. Nandonde

Akizungumzia miundombinu ya shamba hilo, Dkt. Nandonde amesema hajaridhishwa na hali ilivyo sasa kwa kuwa mifugo iliyopo shambani hapo ambayo ng’ombe ni 295 na mbuzi 64 bado ni michache na haifugwi katika maeneo yaliyo rasmi ya uchungaji ambapo amesema nia ya serikali katika kipindi cha miaka kumi idadi ya ng’ombe katika shamba hilo ifike Elfu Moja, huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendela na mikakati ya kuboresha zaidi miundombinu ya shamba.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shamba la Nangaramo Bw. Salum Kamota amesema kwa sasa shamba hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wananchi wengi kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wamekuwa wakihitaji kununua ng’ombe bora na kisasa ili kufuga kwa tija na kupata matokeo mazuri yakiwemo ya upatikanaji wa maziwa mengi kutoka katika ng’ombe hao kwa kuwa shughuli nyingi za kiuchumi zimeongezeka katika mikoa hiyo na kusababisha ongezeko la watu na mahitaji yao.

“Shamba hili ni pekee katika ukanda huu wa kusini hivyo juhudi za haraka zinahitajika kuongeza uzalishaji zaidi wa shamba hili kutokana na mahitaji ya ng’ombe bora wa kisasa katika ukanda huu kutokana na kukua kwa shughuli nyingi za uchumi kwa ukanda huu wa kusini hivyo hamasa ya ufugaji imeongezeka na soko la mazao ya mifugo limekuwa likikua siku hadi siku.” Amesema Bw. Kamota

Shamba la Kuzalisha Mifugo la Nangaramo lililopo katika Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara ni kati ya mashamba matano yanayomilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambapo yamekuwa yakizalisha ng’ombe bora wa kisasa na kuuza kwa wananchi kwa bei nafuu ili waweze kufuga kisasa na kupata mazao mazuri kutoka katika ng’ombe hao.

Mwisho.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post