KUTANA NA MTANZANIA WA KWANZA KUWA AFISA MKUU WA FEDHA,TIGO TANZANIA

Tigo Tanzania ni kampuni inayoongoza katika kubuni, na kuleta huduma na bidhaa bora zinakata kiu ya watanzania, sasa kutana na Innocent Rwetabura mtanzania wa kwanza kuwa Afisa Mkuu wa Fedha

Historia ya bwana Rwetabura inajieleza yenyewe. Alijiunga na kampuni ya Tigo akiwa na uzoefu mkubwa unaotokana na kutumikia katika nyadhifa mbalimbali za juu katika makampuni mengine katika sekta ya mawasiliano. 
Kwa mujibu wa maelezo yake, uhasibu upo katika damu yake. Ndio ni ukweli kwamba uhasibu unaambatana na donge nono, lakini hamasa yake haitokani na malipo au mafao yatokanayo na taaluma hiyo, bali hamasa na msukumo wa kuwa mhasibu mahiri unatokana na ukweli kwamba kazi hii inasisimua kitaaluma. 
Safari yake katika sekta ya uhasibu na fedha ilianza pale alipochukuliwa kwenda kufanya kazi mara baada ya kuhitimu kutoka katika chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1998. 
Kwa mara ya kwanza kabisa aliingia katika sekta ya ajira kama mhasibu msaidizi wa benki, Citibank. Akiwa na miezi michache tu tangu kuajiriwa, Price water house Coopers (PwC) walimpigia simu ya kutaka kufanya naye kazi na akachukua fursa hiyo. “Japokuwa mazingira na mafao yalikuwa mazuri sana pale Citibank lakini matarajio aliyokuwa nayo kwa kufanyakazi PwC yalikuwa bora zaidi. Nilihitaji kuwa pale ambapo utendaji upo. PwC ilikuwa ni njia yangu ya kuelekea kuwa mhasibu mahiri katika mazingira ambayo yanatoa kiwango cha juu cha utaalamu wa uhasibu,” alisema bwana Rwetabura. 
Ni wazi kabisa kwamba bwana Rwetabura ni mtu mwenye malengo makubwa. Ametumikia makampuni mbalimbali akiwa katika nyadhifa mbalimbali kwa miaka mingi. Amefanya kazi na PwC kwa takribani miaka miwili. Baada ya hapo alihamia katika kampuni ya Celtel (ambayo kwa sasa ni Airtel) kama Meneja wa Fedha akitokea kuwa Mkaguzi wa Mahesabu. Alipoanza kazi kama Meneja wa Fedha, kampuni ya Celtel ilikuwa ni ndogo. Kadri ambavyo kampuni hiyo ilivyokuwa inakua, nafasi yake ilipandishwa hadi kufikia kuwa Mdhibiti wa Fedha. 
Baada ya mwaka mmoja na nusu, alihamishiwa nchini Sierra Leone akitumikia kampuni hiyo hiyo na katika wadhifa huo huo wa Mdhibiti wa Fedha. Alifanikiwa kupanda vyeo mbalimbali na kufikia ngazi ya Mdhibiti wa Fedha baada ya mwaka mmoja. 
Mafanikio yake haya hajayapata pasipokuwa na gharama yoyote. “Sierra Leone ni nchi ambayo ilitokea vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kutokana na mtazamo mbaya uliokuwa unasambazwa wakati huo katika vyombo vya habari wakati huo, ilikuwa ni changamoto kwa mke wangu na familia kufwatana na mimi japo kuwa alikuwa akinitembelea mara kwa mara,” Alisema bwana Rwetabura. 
Baada ya miaka mitatu, mwaka 2010, bwana Rwetabura aliona kwamba ni wakati mwafaka wa kurudi Tanzania. 
Alipowasili, alijiunga na kampuni ya Zantel kama Mkurugenzi wa Fedha. Alishikilia wadhifa huu kwa karibia miaka miwili kabla ya kuhamia katika kampuni ya ulinzi ya G4S. Sababu zilizopelekea kuhama ni kwamba aliahidiwa kuchukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji, nafasi ambayo hakupewa. 
Baada ya hapo aliachana na kampuni ya ulinzi na kujiunga na kampuni ya Helios Towers japo katika ngazi za chini. Baada ya muda, kampuni hiyo iliamua kuunganisha vitengo vya idara ya fedha na hivyo nafasi yake iliondolewa. 
Bwana Rwetabura alipewa muda wa miezi sita kuweka sawa mambo yake. Wakati bado anapangilia hatua inayofwata, kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania ilimpigia simu na ilipofika mwaka 2015 safari yake yenye mafanikio na kampuni ya simu ya Tigo Tanzania ilianza rasmi. 
Maisha yake katika kampuni ya Tigo
Awali kabisa bwana Rwetabura alishikilia wadhifa wa Mdhibiti wa Fedha katika kampuni ya Tigo. Mwenendo wake binafsi pamoja na taaluma yake ulichangia kwa kiasi kikubwa katika kumteua bwana Rwetabura kushika nafasi ya Afisa Mkuu wa Fedha (CFO). Amekuwa na mafanikio makubwa tangu alipojiunga na kampuni ya Tigo ikiwemo kuongeza ufanisi kwenye matumizi (Operating Expenditure (OPEX) kwa kiwango ambacho kilikuza faida ya kampuni. Timu anayoiongoza ya idara ya Fedha, iliunganisha kwa wakati mifumo ya Tigo na mfumo wa serikali wa ukusanyaji mapato (ERCS), hatua ambayo imesaidia mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi na ushuru wa bidhaa kielektroniki.  
“Kazi kubwa ya CFO ni kulinda na kusimamia rasilimali za wanahisa na kuhakikisha maslahi yao yanalindwa na kufwatwa. Jukumu hili linajumuisha kiwango kikubwa cha uwekaji wa mikakati, utekelezaji, usimamizi na uendeshaji wa shughuli zote za kifedha za kampuni ikiwepo kuandaa bajeti na kusimamia utekelezaji wake,” alisema bwana Rwetabura 
“Wakati mwingine CFO anajiona kama mpinzani wa Mkurugenzi Mtendaji na wakati huo huo, mshirika muhimu. CEO na timu yake ya biashara wanaweza kuja na wazo, Ili wazo hilo litekelezwa CFO anakiwa kukubaliana nalo au kuja na wazo mbadala ambalo ni bora zaidi. Kwa muda mrefu CFO wameokuwa wakionekana kama wapinzani. Lakini kwa sasa CFO wameanza kubadilika na kushirikiana na mfumo mzima kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa manufaa ya kampuni na wanahisa,” Aliongeza. 
Ni dhahiri kuwa, mazingira ya usimamizi wa fedha yanabadilika sana na ni muhimu kukidhi viwango vilivyowekwa duniani. Matumizi ya teknolojia za kisasa ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kubaini viashiria vya hatari kwa wakati. 
“Tunapaswa kuendana na kasi hii ya mabadiliko kama tunataka kusonga mbele. Kwa mfano, taarifa zetu za fedha zinapaswa kukidhi viwango vya utoaji wa taarifa za kifedha vya kimataifa. (International Reporting Standards)Kwa hiyo, kuwa na timu yenye weledi sio tu katika idara ya fedha lakini pia katika kampuni nzima ni jambo la muhimu.” alisema Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post