TANZANIA NA MISRI ZAANZA MIKAKATI YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NGOZI

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Misri ambao wamefika hapa nchini kwa nia ya kuwekeza katika sekta ya ngozi na kukubaliana na baadhi ya mikakati ili uwekezaji watakaoufanya nchini uwe na tija kwao na taifa.


Akizungumza ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Naibu Waziri Ulega amesema ujio wa wawekezaji hao wakubwa nchini Misri, ambao umeongozwa na mshauri wa waziri wa viwanda na biashara nchini Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata ngozi Cairo for Investment and Development Mhandisi Yasser El Maghraby, umeonesha utayari mkubwa wa kuwekeza hapa nchini katika sekta ya ngozi kutokana na uwepo wa ngozi nyingi na bora.

“Tumepata wageni ambao wamekuja kuona maendeleo ya sekta ya ngozi nchini wawekezaji hawa ni wakubwa katika biashara ya ngozi nchini Misri, sisi kama taifa bado hatujafaidika vya kutosha na zao la ngozi, tumekuwa tukizalisha takriban vipande vya ngozi ya ng’ombe milioni nne na mbuzi milioni tano kwa mwaka, lakini kuvibadilisha kuviweka katika bidhaa mbalimbali kama vile viatu, mabegi na mikanda bado ni changamoto na ngozi nyingi bado inaharibika katika maeneo ya vijijini kwa hiyo wenzetu hawa wamekuja kutuunga mkono.” Amesema Mhe. Ulega

Naibu Waziri Ulega amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa jitihada anazozifanya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vinavyochakata mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aidha amefafanua kuwa ziara ya wawekezaji hao wakubwa katika biashara ya ngozi nchini Misri, Bw. Mahmoud Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery na Bw. Hisham Gazar Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Piel Color ni mwendelezo wa nchi ya Misri na Tanzania kuwa katika historia na mahusiano mazuri tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambapo kwa sasa mahusiano  hayo yamekuwa yakiimarishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

Naibu Waziri Ulega ameishukuru pia serikali ya Misri kwa kutuma timu hiyo ya wawekezaji ikiongozwa na mshauri wa waziri wa viwanda na biashara nchini humo kufuatia ziara ya kikazi aliyoifanya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa nchini Misri kuanzia tarehe 8 hadi 10 Mwezi Julai Mwaka 2019 ambapo alitembelea mji wa viwanda vya ngozi Roubiki na kuzungumza na wazalishaji wa bidhaa za ngozi nchini humo na kuwapa mwaliko wa kuja nchini Tanzania kuwekeza katika sekta ya ngozi kutokana na ubora wa bidhaa ya ngozi inayopatikana hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo kati ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na wawekezaji kutoka Misri, wawekezaji hao wamemweleza Naibu Waziri Ulega kuwa wameshuhudia ngozi na bidhaa zinazotengenezwa kwa ngozi zikiwa katika ubora ambao unawapa hamasa ya kutaka kuwekeza nchini.

Mmoja wa wawekezaji hao kutoka Misri Bw. Mahmoud Sargy ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery ambacho ni moja ya viwanda vinavyosafirisha kwa wingi ngozi kwenda nje ya nchi ameiomba serikali ya Tanzania kuendelea kuunga mkono sekta binafsi na kwamba ili waweze kunufaika kupitia uwekezaji ambao wataufanya hapa nchini, wanatarajia serikali itawawekea mazingira mazuri ya uwekezaji ili uwe na tija kwao na taifa.

“Serikali ya Tanzania lazima itupe ushirikiano katika uwekezaji huu na likifanyika hilo sisi tunaweza kuendelea, tuna uzoefu, tuna masoko ya bidhaa zetu tumekuwa tukifanya biashara hii nchini Misri kwa muda mrefu na tayari tunasafirisha ngozi iliyochakatwa pamoja na bidhaa za ngozi katika bara la ulaya, Mashariki ya mbali, Amerika na tuna viwanda vizuri vya kisasa nchini Misri ambavyo unaweza kuvifananisha na vingine vilivyopo popote duniani.” Amesema Bw. Sargy  

Wawekezaji hao katika sekta ya ngozi nchini Misri wamehitimisha ziara yao ya siku mbili katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokuwa na lengo la kuangalia fursa zilizopo katika sekta ya ngozi hapa nchini na kujionea maeneo ambayo wataweza kuwekeza.

Katika ziara hiyo, wakiwa jijini Dar es Salaam wawekezaji hao walipata fursa ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Ace Leather Bw. Onorato Garavaglia, ambapo walitaka kufahamu pia namna kiwanda hicho kinavyopata ngozi na hatua inazopitia hadi kuchakata ngozi hiyo kabla ya kuipeleka sokoni pamoja na kukitembelea kiwanda hicho kilichopo Mjini Morogoro na kushuhudia namna ngozi inavyochakatwa kiwandani hapo.

Aidha wametembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi WOISO kilichopo eneo la Salasala jijini Dar es Salaam wakiwa na lengo la kujionea namna ngozi inavyotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali na kushuhudia idadi kubwa ya vijana walioajiriwa wakiwa katika majukumu yao ya kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, mikanda na mabegi ambapo walitaka kufahamu utendaji kazi wa kiwanda, teknolojia zinazotumika kiwandani hapo pamoja na soko la bidhaa hizo ili kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana na wawekezaji waliopo hapa nchini katika sekta ya ngozi.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527