BODI YA SHIRECU YATUMBULIWA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA,MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) Richard Luhende akipinga taarifa ya uchunguzi kuhusu ubadhirifu SHIRECU- Picha na Kareny Masasy Malunde1 blog

Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Richard Luhende imevunjwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa shilingi millioni 8.97  pamoja na kutumia fedha zingine kinyume cha utaratibu ikiwemo kuweka mhasibu mkuu hewa aliyelipwa kiasi cha shilingi 770,000/=  ndani ya siku kumi.

Bodi hiyo imevunjwa rasmi Jumamosi Agosti 10,2019 na Mrajisi Msaidizi kutoka Vyama vya Ushirika Tanzania ,Josephat Kisamalala wakati akiongoza mkutano mkuu wa SHIRECU baada ya wajumbe 120 waliohudhuria kupiga kura ya kuwakubali au kuwakataa ambapo wajumbe 99 wakiikataa bodi hiyo kuendelea kuwaongoza.

Bodi hiyo ilikuwa ikiongozwa na Richard Luhende (Mwenyekiti), Enock Lyela (makamu mwenyekiti) na Donald Rogers,Dotto Kangoka na Jeremiah Kapolo(wajumbe).

Baada ya bodi hiyo kuvunjwa yalichaguliwa majina ya wajumbe wapya saba ambao watachunguzwa na watano wakaobaki ndiyo watakaounda bodi ili kuongoza chama hicho.

Mkaguzi Mwandamizi kutoka COASCO makao makuu Dodoma Gabriel Msuya alisema agizo la ukaguzi lilitoka kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kuanzia tarehe 19 Novemba mwaka 2018 hadi tarehe 25 Novemba mwaka 2018 walibaini shilingi millioni 8,976,880 za ukarabati wa magari makubwa zilizotumika bila idhini ya mkutano mkuu na kibali cha mrajisi wa vyama vya ushirika.

Pia Msuya alisema katika zoezi la ukarabati wa majengo walibaini dosari kutoandikwa barua kwa mrajisi na shilingi 71,866,100/= zilitumika bila kuidhinishwa sanjari na mfanyakazi Paul Mainga kuwa katika nafasi ya uhasibu mkuu kinyume cha utaratibu na kulipwa kiasi cha shilingi 770,000/=.

Msuya alisema waliangalia uhalali wa fedha zilizotumika katika kulipia matangulizi ya matrekta matatu kiasi cha shilingi 36,000,000 ikiwa ilibaini vyama vitatu pekee vyenye viongozi wake wajumbe wa bodi ndiyo wangekuwa na uwezo wakupata matrekta hayo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack alisema kuwa SHIRECU sio taasisi ya mtu mmoja ,serikali iliamua kufufua vyama vya ushirika ili kuwasaidia wakulima na kusimamiwa na mkuu wa mkoa hivyo wajue wanaotenda maovu wako mlangoni mwa jeshi la polisi kwani unatakiwa uaminifu na uadilifu kwa watu wanaowasimamia.

Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) waliotumbuliwa wakiwa ukumbini.Picha zote na Kareny Masasy Malunde1 blog
Wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa SHIRECU wakiwa ukumbini
Mrajisi Msaidizi kutoka Vyama vya Ushirika Tanzania ,Josephat Kisamalala akiongoza mkutano mkuu wa SHIRECU.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akizungumza kwenye mkutano wa SHIRECU 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527