VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WAONYWA KURUBUNI WANANCHI KWENYE UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Limbe Benard Limbe

Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog 
Katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, viongozi wa vyama vya siasa mkoani Kagera wameonywa kutowarubuni wananchi kwa jambo lolote kwani ni kosa kisheria na haki hainunuliwi hivyo atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.

Onyo hilo limetolewa leo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Limbe Benard Limbe wakati akitoa ufafanuzi juu ya taratibu katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Limbe amesema haki ya kuongozwa, haki ya kuchagua na ya kuchaguliwa ni haki ambayo iko huru kwa sababu katiba ya nchi inaruhusu mtu achague ama achaguliwe.

Kutokana na hali hiyo amewaonya wanasiasa kutothubutu kufanya mchezo wa aina yoyote unaolenga kuwarubuni wananchi kwani sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika.

Amebainisha kuwa  kama kuna mtu atajitokeza kumrubuni mwananchi ni kosa kisheria kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni kunyima mwananchi haki yake ya msingi ya kuweza kumchagua kiongozi aliye bora kiongozi ambaye ataweza kumletea maendeleo yake mwenyewe katika kutatua shida zake mbalimbali.

Mkurugenzi huyo amesema wananchi wanapaswa kutochagua kiongozi kwa sababu ya kupewa kitu au msukumu flani bali wachague kiongozi atakayewafaa.

Amesema wananchi wajiandae kufanya uchaguzi wa amani ambapo taratibu na miongozi yote itatolewa na serikali na kuwa itakapowafikia wataiwasilisha katika vitongoji, mitaa na kata na kila mhusika atapata taarifa inayostahili ili zoezi hilo liende katika hali inayotakiwa.

Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo amesema suala la uchaguzi litahusu Mtanzania halisi yaani Raia awe wa kuzaliwa.

"Atakayehusika katika zoezi hilo ni yule aliyeandikishwa na akapewa Utanzania sio kwamba mtu amekuja kufanya kazi na anataka kupiga kura jambo hilo halitakubaliki", amesema

Limbe amesema wananchi wasiwe na hofu yoyote kwani Matangazo yatapita kila mahali na kuwa hadi muda huu tayari zoezi la kubainisha wale wote watakaoshughulika na zoezi zima la kuandikisha liko tayari.

Ameeleza kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi mama kwa kuwa shughuli zote zinafanyika katika serikali za mitaa na wale viongozi ndio viongozi wa ngazi ya mwanzo ambao wananchi wanaishi nao na ambao wananchi ni rahisi kuwafikia.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kuchagua kiongozi aliye bora, kiongozi ambaye anaweza kuyaona matatizo ya wananchi kiongozi ambaye yuko tayari kuyatetea, kuyaona matatizo kwa kufuata sheria taratibu na kanuni. 

Aidha amesema miongozo na taratibu ya katiba imewapa muda mwingine tena wa kubainisha kiongozi wanayemtaka na ambaye ni bora ambaye ataweza kutatua mahitaji yao.

Mkurugenzi huyo amempongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwa jinsi ambavyo amewashirikisha wadau mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa huku akiwataka wananchi kuondoa wasiwasi kwani serikali imejipanga ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa bora.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post