WAKULIMA WA NDIZI,PARACHICHI KAGERA WATAKIWA KUCHANGAMKIA SOKO UGANDA




Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Bukoba

Wakulima wa zao la ndizi mkoani Kagera wametakiwa kuchangamkia fursa ya mazao ya kilimo cha ndizi pamoja na upandaji wa miti ya parachichi kutokana na mazao hayo kuwa na soko kubwa la kiuchumi nchini Uganda.


Kauli hiyo imetolewa na jana Agosti 12,2019 na Balozi wa  Tanzania nchini Uganda Bwana Azizi Mlima wakati akitoa salamu za ubalozi wa Uganda katika mkutano wa wiki ya Uwekezaji Kagera ambao umewaunganisha  wafanyabiashara wa Tanzania (Kagera) na wafanyabiashara wa kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Burundi,  Rwanda Uganda na Kenya katika Ukumbi wa ELCT uliopo katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Mlima alisema uchumi wa Uganda umekua kwa 6% huku mazao ya kilimo cha ndizi na parachichi yakiwa na soko kubwa kiuchumi nchini humo ukilinganisha na nchi nyingine.

Kutokana na mazao hayo kuonekana kuwa na soko la kutosha  nchini Uganda hivyo  Balozi huyo aliwahimiza wakulima wa mazao hayo mkoani Kagera kulima kilimo kwani soko hilo linaweza kumkomboa Mtanzania kutoka katika hali ya umaskini.

Alisema kutokana na mkoa wa Kagera kupendeza na kuonekana wa rangi ya kijani lazima kijani hiyo ionekane katika ubora wa upandaji  miti ya maparachichi ambapo alisema nchini Uganda kilo moja ya parachichi huuzwa kwa shilingi 1200 hadi 1300.

Kuhusu suala la ugonjwa wa mnyauko wa migomba ambao unasumbua zao la ndizi mkoani Kagera,Mlima aliwataka wana Kagera kujitahidi kupambana ili kuutokomeza kwani nchini Uganda haupo kabisa.

Hata hivyo balozi huyo alimpongeza mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Elisha Marco Gaguti katika jitihada anazozifanya za kimaendeleo ambazo zimeubadili mkoa huo huku akitaja ushirikiano uliopo kati ya nchi ya Tanzania na Uganda kuwa wa kuridhisha ambao umeunganishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumtembelea Rais wa Uganda Yoeri Museveni na kubadilishana mawazo yenye kuleta tija kwa wananchi wa pande zote mbili.

Alizitaja fursa zingine za kiuchumi zilizopo nchini humo kuwa ni fursa ya elimu ya Chuo Kikuu kuwa na unafuu sana na yenye ubora , fursa ya Bandari ya Dar es salaam – Uganda , fursa za kitalii, bomba la mafuta na bomba la gesi usafiri wa anga utokao Dar es salaam  Kia -Entebe nchini humo.

Wiki ya uwekezaji Kagera yenye lengo la kutangaza fursa zilizopo mkoani Kagera imeanza Agosti 12 mwaka huu itamalizika rasmi Agosti 17 mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527