KANYASU AZIAGIZA TAASISI ZA UHIFADHI NCHINI KUUNDA VIKOSI MAALUM VYA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameagiza kila Taasisi ya Uhifadhi nchini ihakikishe inaunda kikosi maalum cha askari wanyamapori watakaokuwa wakitumika kudhibiti wanyama wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi ya wananchi badala ya kutegemea kikosi kimoja p cha  Askari  kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)

Agizo hilo amelitoa jana wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Shamba la miti la Rondo  ikiwa ni ziara yake ya kikazi katika mkoa wa  Lindi.

Akizungumza na watumishi hao, Mhe.Kanyasu amesema kutokana na Serikali kudhibiti ujangili kwa kiasi kikubwa wanyamapori kama vile tembo, chui na simba  wamekuwa wakitembea kila mahali kwa sababu hawana hofu ya kuuliwa kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Amesema hali hiyo imepelekea mazao pamoja na maisha ya wananchi kuwa hatarini hasa kwa wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi.

Amesema licha ya wanyamapori hao kuongezeka ikiwa moja ya sababu ni Serikali  kuzuia kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi wanyama hao wamekuwa wakipita njia zao za asili  ambazo tayari zimevamiwa na hivyo kusababisha matatizo makubwa kwa wananchi.

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Hifadhi za Taifa( TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) ziwe na vikosi maalum vya askari watakaotumika  kukabiliana na wanyamapori hao wakati wanapovamia vijiji.

" Kwa sasa kukutana na kundi la tembo zaidi ya 500 katika miji ya Butiama, Dodoma pamoja Morogoro ni jambo la kawaida, Hatuwezi kutegemea  KDU pekee lazima nguvu iongezwe" alisema Mhe.Kanyasu.

Amesema TFS ihakikishe inakuwa kikosi hicho cha Askari katika Hifadhi za Mazingira Asilia ambako kuna wanyamapori wakali ma waharibifu wakiwemo tembo na viboko, simba na chui.

Amesema kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikipokea maombi mengi kwa siku kutoka kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ametoa pole kwa wananchi wa Kijiji cha Rondo kufuatia kifo cha kumpoteza Mwalimu  wa shule ya msingi pekee katika kijiji hicho  aliyekufa baada ya  kuuliwa na tembo baada ya kumpiga picha tembo aliyekuwa akihangaika kumnasua mtoto wake aliyekuwa amenaswa kwenye kichaka.

Aidha, Mhe.Kanyasu amezitaka Halmashauri nchini zinazopakana na Hifadhi zihakikishe zinaajiri askari Wanyamapori watakaokuwa wakisaidia kutoa msaada wa haraka pindi wanyamapori hao wanapovamia vijiji

Pia, Amezitaka Halmashauri ziangalie uwezekano wa kuwatumia askari wanyamapori wa vijiji (VGS) kwa kuandaa utaratibu maalum wa kuwakabidhi silaha pindi wanyamapori wanapovamia mashamba na makazi ya wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Mgenda amesema kutokana na juhudi za uhifadhi unaofanywa na Mkoa huo umechangia wanyamapori kuongezeka na kuwa huru kutembea kila mahali

Kufuatia na hali hiyo, Mhe. amemuomba Naibu Waziri huyo ahakikishe  Taasisi zake za  Uhifadhi nchini zunatoa elimu kwa wananchi ili waweze kujihami wakati wanyamapori hao wanavamia mali na makazi yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post