NAIBU WAZIRI KANYASU AIAGIZA TFS IDHIBITI WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KUPANUA MAENEO YA UCHIMBAJI KATIKA SHAMBA LA MITI LA BIHARAMULO-CHATO


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) kupitia Menejimenti ya Shamba la Miti la Biharamulo- Chato mkoani Geita idhibiti upanuzi wa Uchimbaji madini unaofanywa na Wachimbaji wadogo nje ya yale maeneo ambayo yanatambulika kwa shughuli hiyo katika Shamba hilo.

Aidha, Mhe.Kanyasu ameiagiza TFS idhibiti uanzishwaji wa makazi mapya pamoja na ukataji ovyo wa miti unaoendelea hadi pale Kamati ya Mawaziri nane itakapotoa ripoti iliyokuwa imeundwa na Rais John Pombe Magufuli kufuatia maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na wilaya ya Chato kupitia Mbunge wao, Dkt. Medard Kalemani ya kuomba ardhi yenye ukubwa wa hekta 25 nje ya hifadhi hiyo ili kuwawezesha Wachimbaji hao kuanzisha makazi yao ya kudumu.

Hatua hiyo inakuja kufuatia uwepo wa leseni saba zilizotolewa na Wizara ya madini na kati ya hizo saba ni leseni moja tu ndo ambayo imeshalipiwa kibali cha kufanya shughuli hiyo ndani ya Shamba hilo

Agizo hilo amelitoa leo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wapatao 2000 katika eneo la Matabe ndani ya Shamba hilo, na kuwataka Wachimbaji hao wafuate sheria na taratibu zinazotakiwa za kuchimba madini ndani ya shamba hilo.

Katika shamba hilo Wachimbaji wadogo wamekutwa wakiendelea kuchimba dhahabu katika eneo la Matabe, Ilyamchele na Nyantimba ambapo wengi wao wakiwa hawana leseni wala kibali cha kuchimba kutoka TFS.

Amewataka Wachimbaji hao wajiunge katika vikundi visivyopungua watu watano ili waweze kukidhi vigezo vya kupewa leseni na badaye
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) itoe kibali cha kuwawezesha kufanya tathmini katika maeneo ya leseni hiyo.

Amesema kitendo cha Wachimbaji hao kukosa vibali vya kuchimba madini ndani yua Shamba hilo kunaikosesha serikali mapato kwa vile hawatambuliki.

Aidha, Mhe.Kanyasu amewaonya wachimbaji hao kuacha tabia ya kukata miti ovyo kwa ajili ya shughuli za machimbo pasipo kuomba kibali kutoka TFS

” Tutakapokubaini unakata miti kwa ajili ya machimbo tutachukua sheria kali dhidi yako kwa kulipa faini au jela miaka miwili” alilisitiza Kanyasu.

Kwa upande wake Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Madini, Dkt.Medard Kalemani amewaeleza Wachimbaji hao kuwa nia ya serikali sio kutaka kuwafukuza ila inawataka wafuate sheria na taratibu ili waweze kutambulika na serikali

” Serikali inataka ninyi Wachimbaji wadogo mnufaike wakati huo huo Serikali nayo inufaike hivyo lazima mjiunge kwenye vikundi ili mtambulike kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhandisi.Mtemi Msafiri amewaonya Iponya Nybihabi wanaodai kuwa wao ndo wamiliki wa leseni waache kuwasumbua Wachimbaji wadogo kwani ofisi yake haiwatambui

Kufuatia malalamiko mengi kutoka Wachimbaji wadogo kuwalalamikia Wachimbaji hao Wakubwa, Mkuu wa wilaya hiyo alilazimika kumuamuru Mkuu wa Polisi kuwakamata Wachimbaji hao wakubwa na kisha kuondoka nao.

Naye ,Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Emanuel Juang amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa licha ya kusumbuliwa mara kwa mara na Wachimbaji Wakubwa katika eneo la Mataba lakini wapo tayari kufuata sheria na taratibu zinazotakiwa ikiwemo suala kununua miti kwa TFS kwa ajili ya uchimbaji madini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post