MSEMAJI MKUU WA SERIKALI AWAPONGEZA WAANDISHI WA HABARI WANAORIPOTI MKUTANO WA SADC


Mkurugenzi wa Idara ya habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amewapongeza wanahabari wote wanaoripoti shughuli mbalimbali za mikutano ya wiki ya SADC kuanzia ufunguzi , wiki ya viwanda na hata mikutano ya ndani inayoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Abbasi amesema tangu kufunguliwa kwa mikutano ya SADC wanahabari wamekua mstari wa mbele kuuhabarisha umma juu ya matukio mbalimbali yanayoendelea, lakini pia kufanya shughuli za mikutano zinazoendelea zifahamike kwa umma wa watanzania.

“Nitakua mchoyo wa fadhila kama sitatambua mchango wenu kwa jinsi mnavyojitoa kufanya kazi kwa weledi lakini pia kwa uzalendo mkubwa na mapenzi kwa nchi yenu, hii inaonyesha jinsi watanzania tulivyo wamoja na makini hasa yanapokuja masuala muhimu ya kitaifa” Alisema Dkt.Abbasi.

Amesema japo mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali haujafanyika, kazi kubwa zimefanywa na wanahabari kuanzia wiki ya viwanda hadi leo ambapo Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.Palamagamba Kabudi amekabidhiwa uenyekiti wa baraza la Mawaziri la SADC.

Kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na wanahabari, Dkt Abbasi amesema wataandaa tuzo kwa wanahabari hao baada ya kumalizika kwa mkutano Mkuu wa 39 wa nchi za SADC ili kuwapa motisha na pia kutambua mchango wao walioutoa kwa nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post