MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA SHINYANGA ATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI KUJENGA VYUMBA VYA MADARASA

Mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga ametakiwa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Shikizi ya Iyogelo iliyopo katika kata ya Lyamidati halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ili kuwasaidi watoto kusoma katika shule hiyo.

Agizo hilo limetolewa leo Agosti 21, 2019 na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza katika ukaguzi wa vyumba vya madarasa ya shule hiyo, na kusema kuwa fedha iliyopatikana kutokana na mauzo ya pamba itumike kumalizia shule hiyo.

"Nimuombe Mkurugenzi kwa sababu yupo, safari hii tumeuza Pamba na tumepata fedha kutokana na ushuru wa pamba, angalia namna bora ya kukamilisha ujenzi huu ukishirikiana na wananchi", amesema Telack.

Pia ametaka eneo hilo la shule liwekewe mipaka ili lisije likavamiwa na watu na kusababisha migogoro.

"Kijiji kimetoa eneo ni vizuri tukahakikisha kwamba tunaweka mipaka ili tusirudi nyuma na kugombana na wananchi waliotoa ardhi hii kwamba sasa wanavamia eneo lao la shule", amesema Telack.

Kwa upande wake Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza wananchi kwa jitihada zao za kuchangishana na kujenga shule hiyo.

"Kazi waliyoifanya ya kuchangishana na kuweza kusimamisha majengo haya na baadae kusaidiwa na taasisi nyingine kumalizia, ni jambo la kijasiri sana na ni mwamko mzuri wa kujua faida ya elimu kwa watoto wenu",amesema Balozi Iddi.

"Naomba juhudi hizi ziendelee ili watoto wenu hapa waweze kusoma na hasa hasa watoto wadogo",ameongeza Balozi Iddi.

Aidha ameitaka halmashauri hiyo ijitahidi kumalizia sehemu iliyobaki ya shule hiyo ili watoto waweze kusoma hapo.

Pia amewasisitiza wanafunzi wote katika kata ya Lyamidati kusoma kwa bidii ili itoe wasomi watakaolisaidia taifa hapo baadaye.

"Sio kwasababu mnaitwa Shinyanga Vijijini basi muone hamna uwezo wa kutoa wasomi, tunataka Lyamidati itoe mainjinia, mawaziri na hata marubani, kwanini isiwezekane? Kwani hawa walioweza walifanya kitu gani? Na wao walisoma kama mnavyosoma ninyi",amesema Balozi Iddi.

Katika hatua nyingine ametoa shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo Shikizi ya Iyogelo.

Awali akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa shule hiyo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amesema kwamba zinahitajika shilingi Milioni 25 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Shule hiyo Shikizi ya Iyogelo iliyopo kata ya Lyamidati halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imejengwa kwa ushirikiano wa michango ya wananchi, serikali ya Tanzania na serikali ya Uingereza kupitia (UKAID) kupitia mradi wa EQUIP Tanzania na ipo chini ya usimamizi wa shule mama ya Ihugi.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 41 wasichana 18 na wavulana 23 na inachukua wanafunzi wa darasa la wali hadi darasa la pili.

Kabla ya kujengwa shule hiyo watoto wa kijiji cha Iyogelo walikuwa wakitembea umbali mrefu wa takribani kilomita tano mpaka kufika shule ya Msingi Ihugi kwa ajili ya masomo, na kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo ya Iyogelo itawasaidia watoto wadogo kupata elimu katika mazingira mazuri na kutotembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Na Annastazia Paul - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post