MAREHEMU ALIYEZIKWA NA TAI,VIATU AZUA BALAA.....'ANATAKA AZIKWE UPYA'


Huenda familia moja kutoka eneo la Ikolomani, kaunti ya Kakamega nchini Kenya ikafukua maiti ya jamaa wao waliyemzika kufuatia ripoti kwamba alikuwa anawahangaisha kwa kutozingatia utaratibu wakati wa mazishi yake.


 Inasemekana marehemu Pius Shipanda Shitsukane, ambaye alihudumu kama naibu wa chifu katika mtaa wa Shiseso na aliyezikwa hizi majuzi, amekuwa akiwahangaisha jamaa zake na kutaka mwili wake ufukuliwe. 

Inaelezwa kuwa Mkewe Shipanda amekuwa akiugua tangu kuzikwa kwa mumewe na wazee wa jamii wamedai maradhi yanayomkumba yamesababishwa na gadhabu ya mumewe.

Pius Shipanda alidaiwa kuzikwa akiwa amevishwa viatu na tai kinyume na mila na desturi za jamii ambapo baadhi ya jamaa wa familia hiyo walidai wamekuwa wakikumbwa na masaibu katika nyumba yao tangu jamaa huyo azikwe.

Duru zinaarifu kwamba, marehemu alivishwa viatu na tai na kisha rungu ambayo alipenda kutembea nayo haswa wakati akihudhuria vikao vya wanaume wa kikatoliki ikatiwa katika sanduku lake kabla ya kuzikwa.

 Pindi tu baada ya mazishi yake katika boma lake kijijini Ikhumbula-Ibukhubi, mkewe alianza kuugua na kulazwa hospitalini.

 Hata hivyo, wakazi wanaamini chifu huyo ndiye chanzo cha mkewe kuugua kwa kuwa alikuwa hajafurahishwa na mazishi yake. 

 "Ni kinyume na mila za jamii ya Luhya kumzika marehemu na bidhaa kama vile tai, saa, pesa, shanga, chupi au soski," Lawrence Alusiola ambaye ni mzee wa jamii alisema.

 Alisema wale wote ambao wamekiuka tamaduni hiyo wamepokea adhabu na kulazimika kuufukua mwili ili kuondoa vifaa alivyozikwa navyo marehemu. 

 "Tumeshuhudia visa kama hivyo kwa miaka ya hapo awali. Unapata familia inakiuka desturi zetu na kusisitiza kuwazika wapendwa wao jinsi wanavyotaka kisha wanajuta baadaye wakati wanapotatizwa na marehemu," Elias Khwani mzee mwingine kutoka jamii hiyo alisema.

 Inadaiwa, marehemu Shipanda amekuwa akiwatatatiza jamaa wa familia yake haswa nyakati za usiku akitaka tai, viatu na rungu aliyozikwa navyo ziondolewe.

"Maradhia ambayo yamemkumba mkewe ghafla yanahusikana na marehemu kwa kuwa baadhi ya wanachama wa kikundi cha wanaume wa kikatoliki walikataa kusikiza ushauri wa wazee na kumzika marehemu na bidhaa zisizostahili. Ni sharti waufukue mwili au familia itazidi kuhangaika," mzee mwingine wa jamii alitoa tahadhari. 
Via Tuko

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527