MAJERUHI MWINGINE AJALI YA MOROGORO AFARIKI....13 BADO HAWAJITAMBUI NA WAKO ICU


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro  (RC) nchini Tanzania, Dk Stephen Kebwe amesema vifo vinavyotokana na ajali ya mlipuko wa moto iliyotokea Jumamosi iliyopita ya Agosti 10, 2019 mkoani humo vimeongezeka na kufikia 76.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 13,2019 nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, RC Kebwe amesema idadi hiyo imefikia baada ya majeruhi mmoja aliyelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kufariki usiku wa kuamkia leo.

Amesema majeruhi waliosafirishwa kwenda Muhimbili wengi walikuwa katika hali mbaya kwa sehemu kubwa ambapo mpaka sasa (asubuhi) wamebakia 38 wakiendelea na matibabu na katika Hospitali ya Rufaa Morogoro wamebaki 16 nao wakiendelea na matibabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Aligaesha  amesema  Majeruhi 13 kati ya hao  38 walionusurika katika ajali hiyo, waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hali zao bado ni  mbaya na wamelazwa katika Chumba cha wagonjwa Mahututi (ICU) wakiwa hawajitambui.

“Hadi leo Agosti 13, hiyo ndiyo idadi ya wagonjwa waliolazwa MNH, na wale ambao wamefariki tayari miili yao imepelekwa Morogoro na mmoja umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hapa Muhimbili,” amesema Aligaesha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527