LUGOLA AAPA KUENDELEA KUPAMBANA NA POLISI WASIOTII MAAGIZO YAKE


Na Felix Mwagara, MOHA.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola mara baada ya kuteuliwa na Rais Dk John Joseph Pombe Magufuli kuiongoza Wizara hiyo, kazi ya kwanza aliyoifanya ni kulivunja Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na mabaraza yote ya ngazi ya Mkoa nchini.




Waziri Lugola alitangaza uamuzi huo Julai 5, 2018 jijini Mbeya alipozungumza na Wajumbe wa Baraza la usalama barabarani mkoani humo kutokana na changamoto mbalimbali zilizokua zinalikabili Baraza hilo, ikiwemo ongezeko la ajali, na askari wa usalama barabarani kujihusisha na matukio ya kuchukua rushwa.

Kutokana na uboreshaji wa baraza hilo, Lugola anaendelea kuhakikisha matrafiki wanafanya kazi kwa weledi kuepuka rushwa na kutonyanyasa madereva ambao wanafuata taratibu za usalama barabarani.

Licha ya baadhi ya madereva kutii sheria bila kushurutishwa lakini wapo ambao wanavunja sheria za usalama barabarani, Waziri Lugola anawaagiza Polisi nchini kuendelea kuwakamata na kuwapiga faini pamoja na kuwapeleka mahakamani wanaovunja sheria.

Lugola alisema kuna baadhi ya askari wa usalama barabarani wanajua sheria lakini wanafanya makusudi kwa lengo la kupata fedha za rushwa kwa madereva wanaofanya makosa au wana vyombo vya moto ambavyo ni vibovu.

Kutokana na changamoto hizo, Lugola akiwa katika ziara zake za kikazi zilizoambatana na mikutano ya hadhara, alizozifanya kuanzia mwezi Julai, 2019 mara baada ya kuteuliwa kuingoza Wizara hiyo, katika Mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha na Morogoro, licha ya kuzungumza mengi ya Wizara yake, lakini alijikita zaidi kusambaratisha kero za bodaboda nchini.

Lugola anasema yeye hawezi kufanikiwa peke yake bila Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kumpa nguvu anapotoa maagizo yake kwa viongozi wa Jeshi ambapo lengo lake kuu si kubomoa bali kuboresha na kuwafanya madereva wa bodaboda waweze kupambana na hali ngumu ya maisha kupitia biashara ya bodaboda wanaoifanya.

“Lengo langu kuu ni kuwasaidia waendesha bodaboda waweze kufanya kazi zao kwa amani, bila bughudha kama walivyoahidiwa na mheshimiwa Rais Magufuli, hivyo maelekezo ninayotayoa kwa Jeshi lazima yafuatwe,” anasema Lugola.

Lugola amesema baadhi ya Wakuu wa Vikosi vya Usalama Barabarani (MaRTO) wanapuuza maagizo yake wakisema kuwa ni maagizo ya kisiasa hivyo wao wanafuata sheria, hali inayomfanya Waziri huyo kuchukizwa na kauli hizo ambazo zinavunja sheria za nchi na pia yeye Waziri anamamlaka ya kutoa agizo lolote ambalo lipo sahihi kwa mujibu wa sheria.


“Mimi ni Mwanasiasa nikiwa jimboni kwangu Mwibara, nje ya jimbo langu, mimi ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hivyo ninapotoa maelekezo au maagizo ni kutokana na nafasi yangu na lazima yafuatwe ili nchi iweze kusonga mbele,” anasema Lugola.


Akizungumza katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika Uwanja wa Stendi, Wilayani Malinyi, Mkoani Morogoro, ambao ulihudhuriwa na mamia ya wananchi Wilayani humo, Waziri Lugola anatoa ya moyoni jinsi baadhi ya viongozi matrafiki mikoa kuyapuuza maagizo yake anayoyatoa.

Lugola anasema yeye anajua sheria ya usalama barabarani, na yupo Wizarani kwa lengo la kumsaidia Rais katika mapambano ya kuondoa umaskini na nchi kuwa na uchumi wa kati, hivyo sekta ya bodaboda ni muhimu katika mapambano ya kuondoa umaskini.

“Sijawahi kutamka katika mikutano yangu yote ya ndani au ya hadhara, kuwa bodaboda wasikamatwe, bali nasema bodaboda lazima wapewe mazingira mazuri ya kufanya kazi yao bila bugudha, na pia kuyakamata hovyo bodaboda na kuzilundika vituoni kwa makosa ambayo yanapaswa kutozwa faini hilo nimelikataza,” anasema Lugola.

Anasema wapo baadhi ya wakuu wa matrafiki mikoa wanayapuuza maagizo yake na mmojawapo ni RTO Mkoa wa Arusha ambaye anatumia mikutano anayoalikwa kunipinga na kuyaaita maagizo yangu ninayoyatoa kwa maunfaa ya nchi ni yakisiasa.

Lugola kutokana na kumfuatilia RTO huyo kwa muda mrefu, kupitia mkutano wa hadhara wa Mji wa Malinyi, alitamka hadhara kumuondoa madarakani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, Charles Bukombe na kumuagiza Katibu Mkuu, pia kumchukulia hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa matrafiki hao wa mikoa nchini.

Lugola amesema RTO huyo ameshuhudia katika video ambayo ilikua inasambaa mitandaoni akiwa katika mkutano jijini Arusha, akipinga maagizo yake na kuyaita ya kisiasa na pia kutokuyatekeleza.

“Sitoi maagizo ya kisiasa bali anatoa maagizo yatakayomsaidia rais kazi zake kwa wananchi wanyonge wanaopambana na umaskini na ajira, kutokana na kutokuwa na nidhamu kwa RTO huyu namuagiza katibu Mkuu achukue hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumuondoa u-RTO afanye shughuli zingine za kipolisi,” anasema Lugola.

Pia Lugola anatoa onyo kwa RTO wa Mikoa ya Morogoro na Mara, kujitathimini katika utendaji wao, na pia anawataka wakuu wa vikosi hao katika mikoa mbalimbali nchini kuyasimamia vema maagizo yake kwa kutowaonea wananchi, kuacha kuchukua rushwa barabarani.

Lugola anasema Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

Katika Mkutano huo, Lugola anaagiza kuwa, Jeshi katika vituo vya polisi nchini, bodaboda zinazotakiwa kuwepo vituoni ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Ninasisitiza kwa mara nyingine, bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,” anasema Lugola.

Katika kazi ya kuhakikisha madereva wa bodaboda na magari nchini wanafanya kazi zao kwa utulivu bila kunyanyaswa, Januari 2, 2019, akiwa mjini Bukoba, Mkoani Kagera, anatangaza kuwa, gari lolote litakalokamatwa na trafiki kwa kosa la bodi ya gari bovu, weipa haitoa maji, taa za breki haziwaki, mafuta yanavuja, hapo kosa ni moja tu, gari ni bovu na faini ni shilingi 30,000, na si sahihi kuwa kila tatizo la gari ni kosa linalojitegemea.

Huku wananchi wakimshangilia Waziri Lugola katika mkutano huo, aliendelea kusema kuwa, Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

“Kutokana na changamoto za barabarani, nawaagiza polisi wa usalama barabarani nchini, gari lolote litakalokamatwa kwa kosa la bodi ya gari bovu, weipa haitoa maji, taa za breki haziwaki, mafuta yanavuja, hapo kosa ni moja tu, gari ni bovu na faini ni shilingi 30,000, na si sahihi kuwa kila tatizo la gari ni kosa linalojitegemea,” anasema Lugola.

Akiwa Mkoani Arusha, mwezi Februari, 2019, katika Mkutano wake wa hadhara uliofanyika Jimbo la Arumeru, Waziri Lugola anapiga marufuku tabia ya baadhi ya askari Polisi hapa nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za Jeshi, anasema kwa kufanya hilo kunaleta kero kwa madereva na pia anayekamatwa anaweza akadhaniwa kuwa ni jambazi.

Lugola anaongeza hayo katika Mkutano huo wa hadhara uliofanyika uwanja wa Wilayani humo, akisisitiza kuwa, polisi wanapaswa kufuata utaratibu wa kijeshi hasa wanapokamata vyombo vya moto na siyo kuvunja utaratibu.

Lugola anafafanua kuwa, bodaboda zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo.

“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” anasema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda wa Wilaya ya Arumeru, jijini Arusha na Tanzania kwa ujumla wafuate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha vyombo hivyo vya moto wanapaswa kuwasha taa.

WaziriI Lugola licha ya kuzungumza hayo katika mikutano yake ya hadhara, pia anazungumza maneno hayo katika Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa, Wilaya na pia Mikutano yake na askari na watumishi raia wa Wizara yake waliopo mikoani.

Pia Waziri Lugola, anatangaza dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi.

Waziri Lugola anaendelea na ziara ya aina hiyo nchi nzima, na anatarajia Agosti 10, 2019 kuanza ziara Mkoa wa Rukwa ambapo anatarajia kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa huo kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, na pia kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais John Magufuli nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527