KESI YA BENARD MEMBE DHIDI YA CYPRIAN MUSIBA YAKWAMA


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekwama kusikiliza kesi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Benard Membe dhidi ya Cyprian Musiba kwa sababu Jaji hayupo.

Kesi hiyo namba 220 ya mwaka 2018 ilipangwa kusikilizwa leo baada ya pande mbili baina ya mlalamikaji na mlalamikiwa kuwasilisha majibu yao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari nje ya Mahakama Wakili wa Membe, Jonathan Mndeme amesema shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Wakili Mndeme amesema kuwa  shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 3, 2019 mbele ya Msajili kwa sababu Jaji aliyepaswa kusikiliza shauri hilo hayupo.

Katika Kesi hiyo iliyoitwa kwa mara ya kwanza Februari 26, 2019, Membe amemshtaki Musiba, Mhariri wa gazeti la Tanzanite na wachapishaji wa gazeti hilo ambapo anawadai Sh. Bilioni 10 kwa madai wamemchafua.

Musiba katika kesi hiyo anashtakiwa kwa kumtuhumu Membe kuwa anamhujumu Rais John Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020 kupitia CCM.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527