DAKTARI FEKI ATIWA MBARONI MKOANI RUVUMA

Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia Moses Lucas Masoud (34) mkazi wa Visiga mkoani Pwani  kwa tuhuma ya kujifanya daktari bingwa wa kutibu  magonjwa  mbalimbali ya binadamu.


Inadaiwa daktari huyo feki alikuwa akitoa huduma za kitabibu katika Kanisa la Jesus Miracle Church (JMC) lililopo maeneo ya Msamala kwa Gasa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambapo wananchi walimbaini na kutoa taarifa kwa Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Jair  Khanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano Agosti 14, 2019 Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa alisema daktari huyo feki alikamatwa Agosti 13,2019 saa saba mchana katika maeneo ya Msamara kwa Gasa akiendelea na kutoa huduma za kitabibu kwa binadamu.

Alisema kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo ya kitabibu aliingia kwenye kanisa hilo na kujitambulisha yeye ni daktari bingwa ana uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na pia alijitambulisha yeye ni daktari anayetibu viongozi wakubwa wa Serikali ya Tanzania.

Kamanda Maigwa alidai daktari huyo feki  amekuwa akitoa huduma hiyo ya kitatibu kwa gharama kati ya Sh600,000 hadi Sh1.2 milioni kuligana na homa ya mteja wake, kitu ambacho kiliwashtua wananchi na kuanza kumtilia shaka kutokana na gharama ya matibabu ambayo anatoza kwa mgonjwa.

Alisema Polisi akishirikiana na Dk Khanga baada ya kupata taarifa  hiyo walikwenda kwenye kanisa hilo na kumkuta akiendelea kutoa huduma na alipohojiwa alikiri hana taaluma ya udaktari na hajahitimu mafunzo yoyote ya udaktari katika chuo chochote cha udaktari kinachotambulika na Serikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post