CRDB YAWATAKA WANANCHI KUACHA TABIA YA KUWEKEZA PESA KWA WATU BINAFSI WAPELEKE BENKI

Benki ya CRDB tawi la Bukoba mkoani Kagera wamejipanga kutoka elimu kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali hasa akina mama wenye utamaduni kuwekeza fedha zao kwa mtu binafsi jambo ambalo si salama kwa fedha hizo.


 Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 18 , 2019 na Meneja Mwandamizi wa Benki ya CRDB Tawi la Bukoba Karlo A. Sendwa wakati akielezea umuhimu wa kutunza fedha katika Benki ili kuondokana na upotevu wa fedha hizo mara zinapotunzwa kwa mtu binafsi.

Sendwa amesema  kuna utamaduni uliojengeka katika jamii hasa kwa baadhi ya wajasiriamali walio katika makundi mbali mbali hasa ya akina mama juu ya kuwekeza fedha za michango ya makundi hayo kwa mtu binafsi huku wengi wao wakiwa na dhana potofu ya kusema kuwa wanaoenda Benki ni matajiri tu jambo linalosababisha upotevu wa fedha hizo na kufanya maendeleo ya vikundi hivyo kurudi nyuma kutokana na mtu binafsi waliomuwekesha fedha hizo kutoweka nazo.

"Bado kuna watu hawajui umuhimu wa kutumia benki hasa akina mama walioko vijijini, utakuta wanasema pesa yetu ya kikundi anayo fulani jambo hili si salama kwani benki ni mahala salama kwa fedha za mtu", alisema.

Aliahidi utoaji elimu kwa makundi sambamba na kushirikiana nao ili wapate kujua njia sahihi ya utunzaji fedha zao.

Katika hatua nyingine amempongeza mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti pamoja na uongozi wake  kwa kubuni wiki ya uwekezaji kagera kwani Benki hiyo ya CRDB imenufaika na wiki hiyo ambapo amewahimiza wafanya biashara na wakulima kuacha woga katika kuzifikia taasisi za kifedha kwani usalama wa kuwekeza pesa kwa mtu ni sawa na sifuri.

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527