MADIWANI WAMTAKA MKURUGENZI KUFUNGA CCTV KWENYE MAJENGO YA HOSPITALI YA KAHAMA KUDHIBITI UNYANYASAJI WA KIJINSIA


Na Salvatory Ntandu - Malunde1 blog Kahama 
Kutokana na kukithithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa wagonjwa na baadhi ya watumishi wa hospitali ya halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, limemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Anderson Msumba kufunga kamera (CCTV) kwenye wodi zote ili kuwadhibiti tatizo hilo.


Uamuzi huo umetolewa leo kwenye  kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo wamesema,malalamiko ya wagonjwa kutolewa lugha chafu na baadhi ya watumishi hao yamekithiri hivyo  kufungwa kwa kamera hizo itasaidia kupunguza malalamiko hayo.

Hoja hiyo imewasilishwa na diwani kata ya Nyihogo Shedrack Nkwabi na kusema kuwa, endapo mkurugenzi atafunga  kamera katika hospitali hiyo  itasaidia kuwabaini wauguzi au madaktari ambao wamekuwa na tabia ya kufanya ukatili kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo kupata huduma.

 Mbali na hilo Shedrack amesema CCTV hizo zitasaidia kuwabaini baadhi ya watumishi ambao sio waadilifu wanaoiba dawa na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni sambamba na kuwafukuza kazi.

"Mkurugenzi utakapofunga CCTV kwenye wodi itasaidia kupunguza unyanyasaji kwa wagonjwa hasa wanawake unaofanywa na baadhi ya watumishi ambao sio waadirifu.

"Hata wagonjwa akina baba huwa wanafanyiwa vitendo hivyo lakini wanashindwa kutoa taarifa",alisema Nkwabi.

Naye diwani viti maalumu kata ya Malunga Berenadeta Mbagale alisema,asilimia kubwa ya wagonjwa ambao wamekuwa wakirushiwa maneno machafu na wauguzi ni akinamama ukilinganisha na akina baba.

Aidha alisema kuwa,wao kama wawakilishi wa wananchi wamekuwa wakipata malalamiko mengi kutoka kwa wagonjwa kuhusiana na kufanyiwa vitendo hivyo,lakini wamekuwa wakikosa ushahidi wa kuwachukulia hatua kutokana na ushahidi wa maneno badala wa video au sauti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Anderson Msumba alisema,kwa sasa Halmashauri inajenga jengo la kupumzikia wagonjwa wa nje (OPD) na kila wodi na ofisi za madaktari zitafungwa CCTV ili kuweza kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa kiripotiwa na wagonjwa. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post