CCM KAHAMA YANG'OA WANACHAMA WA CHADEMA....MWENYEKITI ATAKA KUCHAGUA VIONGOZI BORA



Na Salvatory Ntandu - Malunde1 blog Kahama
Kuelekea katika uchanguzi wa serikali za mitaa hapa nchini wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuchagua viongozi bora na sio bora kiongozi ambao wataweza kusimamia fedha na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Kahama Thomas Myonga wakati akizungumza kwenye mkutano maalum wa chama hicho wa kuwapokea wanachama sita wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliofanyika katika kijiji cha Ufala kata ya Kilago.

Amesema katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu ni vyema wananchi wakafanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi wenye sifa, wasiokuwa watoa rushwa na walevi ambao siyo waadilifu wanaotaka madaraka kwa maslahi yao binafsi.

Amefafanua kuwa wanachama hao sita wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho Daniel Makoye wamefanya uamuzi sahihi ya kuhamia (CCM) kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Dk John Pombe Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Ameongeza kuwa CCM mpya haina makundi hivyo ni jukumu lao kushirikiana nao katika juhudi za kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi katika uchaguzi huo na mbinu pekee ya kushinda ni pamoja na kuweka wagombea wanaokubalika katika jamii ambao hawana sifa mbaya kama vile walevi,wazembe na wasiopenda kufanya kazi.

Myonga amewakabidhi wanachama hao wapya kadi za CCM ambao ni Daniel Makoye mwenyekiti wa kijiji cha Ufala,Bundala Busuli,Paschal Gulamali,Masanja Peter,Luhende Kaswaki na Hasan Athuman ambao wote walikuwa wanachama wa CHADEMA.

Uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika mwezi Oktoba nchi nzima.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527