SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA MASHINE ZA MCHEZO WA KUBAHATISHA KAHAMA


Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha 

Na Salvatory Ntandu - Malunde1 blog 
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetoa siku saba kwa wamiliki wa mashine za mchezo wa kubahatisha almaarufu (bonanza) kuondoa mashine zao katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha wakati akihutubia baraza la madiwani katika halmashauri ya Ushetu baada ya kupokea malalamiko ya madiwani juu ya uhalifu unafanywa na watu wanaochezesha mchezo huo.

Amesema ofisi yake imebaini kuwepo kwa wamiliki wa mchezo huo kutozingatia sheria na kanuni za uendeshaji kwa jambo ambalo linasababisha watoto kushindwa kuhudhuria masomo shuleni na kujihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo udokozi katika familia zao.

Amefafanua kuwa serikali ya awamu ya tano inahimiza watu kufanya kazi halali ili kujipatia kipato lakini mashine hizo zimekuwa zikisababisha watu kutokufanya kazi kwa wamiliki wake kuzifungua nyakati za asubuhi na kusababisha vijana watu wazima kutowajibika.

”Kila eneo ukipita katika mitaa mbalimbali katika wilaya hii unakuta watu wanacheza bonanza hata kazi za uzalishaji mali hawafanyi serikali isipochukua hatua maadili yataporomoka na tutakuwa tunatengeneza taifa la wezi ambao hawataki kufanya kazi kwa kusubia kubahatisha’’alisema Macha.

Sambamba na hilo Macha amesema mashine hizo zinapaswa kuwekwa katika sehemu za starehe kama vile baa na makasino na hivyo serikali itahakikisha haziwekwi wekwi ovyo katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kama vile katika maeneo ya mitaani ili sheria na kanuni za usimamizi wa michezo huo uzingatiwe.

Wakichangia juu ya hoja hiyo Damasi Joseph diwani wa kata ya chambo na adriano samweli wa kata ya kinamapula katika halmashauri hiyo wamesema mashine hizo zimechangia kuwepo kwa wizi majumbani unafanywa na watoto na watu wazima kutofanya kazi jambo ambalo linapelekea uzoroteshaji wa shughuli za maendeleo.

Wamesema tangu kuingizwa kwa mashine hizo katika halimashauri hiyo vijana,watoto na watu wazima wameshafilisika kutokana na kutokuwa na elimu juu ya mchezo huo hali ambayo inasababisha ofisi zao kupokea malalamiko kutoka kwa wazazi juu ya kuibiwa mali zao.

Ikumbukwe kuwa Sheria ya usimamizi ya michezo ya kubahatisha ya mwaka 2015 inazuia wamiliki wa mashine hizo kuruhusu watoto chini ya umri wa miaka 18 kucheza mchezo huo na inataka mashine hizo ziwekwe kwenye maeneo ya starehe kama vile baa na makasino.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post