Benki Ya Dunia Yaahidi Kuongeza Fedha Mpango Wa TASAF

Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Benki ya Dunia imeahidi kutoa fedha zaidi kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini- TASAF, unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Tanzania kwa kuwa awamu ya kwanza na ya pili ya mpango huo umeonesha matokeo chanya kwa kuboresha maisha ya watanzania kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi 22 zilizopo Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, wakati alipofanya ziara ya kuangalia utekelezaji wa TASAF awamu ya kwanza na ya Pili katika Mtaa wa Keko Machungwa Kata ya Miburani, Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa ameshuhudia mwenyewe wanawake wakiwa wamezalisha bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, vikapu, shanga, mikoba, vyungu, urembo na nguo zilizotengenezwa kupitia mpango wa TASAF, jambo linalodhihilisha manufaa ya mpango huo kwa Kaya masikini katika kukuza uchumi wao.

“Kwa kuwa nawakilisha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika Benki ya Dunia, Washngton Marekani, nimejionea kwa macho yangu bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa hasa na wanawake, hivyo naenda kupeleka ujumbe huo muhimu ili Benki iweze kuongeza fedha zaidi kwa awamu zingine kwa ajili ya mpango huu wa TASAF kutokana na manufaa yake katika kupunguza umasikini nchini Tanzania”, alieleza Bi. Kabagambe.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa  Mtaa wa Keko Machungwa, Bw. Uwessu Misanga, alisema kuwa kuanzia mwaka 2015 hadi Februari, 2019, fedha walizolipwa walengwa wa Kunusuru Kaya Masikini katika eneo lake ni takribani Sh. milioni 86.1.

Alisema manufaa ya mpango huo ni pamoja na upatikanaji wa  mahitaji muhimu kama Chakula, kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni na  kuhudhuria Kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka Kaya Masikini.

Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa kipato kwa walengwa kutokana na biashara ndogondogo zinazofanywa na kaya hizo lakini pia kuboreshwa kwa mahitaji muhimu ya wanafunzi kutokana na ruzuku.

Aidha Bw. Misanga, alibainisha changamoto za utekelezaji wa Mpango wa TASAF kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali, baadhi ya Kaya kukosa fursa ya kuingia kwenye mpango, uhaba wa maeneo ya kufanyia shughuli za kuongeza kipato na pia uhaba wa mitaji katika vikundi vya wajasiriamali vilivyoanzishwa na Kaya hizo.

Alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali inafanya tathmini na mapitio ya mpango kwa awamu ya kwanza ili kuwezesha Kaya zilizoachwa kuingizwa katika mpango huo na pia Ofisi ya Halmashauri ya Temeke Jijini Dar es Salaam, imewaelekeza wanakikundi wa ujasiriamali kuwasilisha mahitaji ya eneo kwa kuzingatia shughuli wanazotaka kufanya ili kutatua changamoto zao.

Baadhi ya wanufaika wa TASAF waliotoa shuhuda zao mbele ya Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, wameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwawezesha kujikwamua kimaisha na pia wameomba kuendelezwa kwa mpango huo kwa kuwahusisha watu wengi zaidi na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post